Poland ondoa kikwazo cha ushiriki COP24

7 Mei 2018

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Poland ihakikishe kila mtu anashiriki ipasavyo mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini humo.

Wataalamu hao wametoa wito huo kufuatia sheria mpya kuhusu usalama na amani nchini Poland ambayo inazuia  ushirikishi wa asasi za kiraia.

Wakizungumza mjini Bonn, Ujerumani wakati maafisa wa serikali ya Poland walipokuwa wanawaelezea  maandalizi ya mkutano huo wa 24, COP24,  wataalamu hao wa masuala ya haki za binadamu wa wameishauri Poland ihakikishe kuwa mkutano huo unashirikisha kila pande.

Tayari wanamazingira wameonyesha wasiwasi wao kuhusu sheria hiyo iliyotungwa kwa ajili ya mkutano huo utakaofanyika nchini Poland, wakisema  itaathiri haki zao za kushiriki kwa amani.

Wataalamu hao wanasema kuwa ili COP24 ifanikiwe, Poland ni sharti iweke mazingira huru kwa washiriki na kuwapa mwanya wanaharakati wa asasi za kiraia kushiriki bila kizuizi, masharti  wala kuchunguzwa.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa   wameihimiza serikali kutoa majibu na maelezo ya kinagaumbaga  kuhusu masuala hayo.

Wamesema kuwa macho yote yameelekezwa Poland, ambayo ni mwenyeji kuona iwapo itaheshimu wajibu wake kuhusu haki za binadamu na kuona kama kunapatikana mazingira ya washiriki wote bila bughudha yeyote.

Ibara ya saba ya sheria hiyo inatoa mamlaka zaidi  kwa polisi na vikosi vya usalama kupata taarifa za washiriki wa mkutano huo na inaruhusu vyombo vya dola  kuwafuatilia wahalifu na baadhi ya watu ambao wanaonekana kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud