Uhifadhi wa tabianchi wazidi kupigiwa chepuo

22 Juni 2018

Mataifa yaliyoendelea yameungana na nchi zingine kuahidi kuweka malengo thabiti zaidi ili kupunguza hewa chafuzi kabla ya mwaka 2020.

Mataifa hayo Ujerumani, Canada, Uingereza na Ufaransa ni miongoni mwa nchi 23

23 zilizotoa ahadi hiyo kupitia taarifa waliyotia saini kwa pamoja na kuipatia jina la azimio la matarajio ni pamoja mwishoni mwa mkutano wao huko Brussels, Ubelgiji.

Azimio hilo linasema kuwa nchi hizo zimeazimia kusaka fursa za kuongeza harakati zao huku likigusia mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mwezi Septemba mwakani.

“Mkutano huo ni fursa kuu zaidi ya kisiasa na tunatoa wito kwa nchi zingine kuungana nasi ili kuelezea nia yao ya kusonga mbele kwenye mwelekeo huu,” limesema azimio hilo.

Mathalani nchi hizo zinalenga kuchagiza uwekezaji mpya kwa kuzingatia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.

Tayari nchi wanachama wa mkataba huo zimeshaahidi dola bilioni 100 kila mwaka ili kusaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

“Tumeazimia kuunga mkono Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika jitihada zake za kuchagiza kasi ya kisiasa kulekea mkutano huo wa Septemba 2019,” limeongeza azimio hilo.

Taarifa hiyo imetolewa mwishoni mwa mkutano wa ngazi ya mawaziri wa nchi za Muungano wa Ulaya pamoja na China na Canada uliohusu mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huo ni wa pili ukileta pamoja wawakilishi kutoka serikali 36 kujadili jinsi ya kusongesha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kabla ya mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi, COP24 utakaofanyika mwezi disemba mwaka huu nchini Poland.

Nchi zingine zilizotia saini taarifa hiyo ni Argentina, Uingereza, Canada, Chile, Colombia, Costa Rica, Denmark, Ethiopia, Fiji, Finland, , Maldives, Visiwa vya Marshall, Mexico, Monaco, Uholanzi, New Zealand, Norway, Rwanda, Saint Lucia, Hispania na Sweden.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter