Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo inaokoa na kuboresha maisha: WHO

Mhudumu wa afya anampatia chanjo mtoto katika kituo cha afya mjini Salamieh huko Hama, kaskazini mwa Homs.
© UNICEF/UN018084/Faour
Mhudumu wa afya anampatia chanjo mtoto katika kituo cha afya mjini Salamieh huko Hama, kaskazini mwa Homs.

Chanjo inaokoa na kuboresha maisha: WHO

Afya

Wiki ya chanjo duniani kwa mwaka 2018 imeng’oa nanga leo  Aprili 24 na itakamilika Aprili 30 .

Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, na wadau wa afya duniani wakiongozwa na shirika la afya ulimwenguni WHO wanahimiza umuhimu wa chanjo sio tu kwa kuokoa maisha lakini pia kwa kuyaboresha.

Ujumbe muhimu wa WHO mwaka huu ni kuhakikisha chanjo inawafikia watu wanaoihitaji zaidi, kuwakinga na kuimarisha afya zao hali ambayo itasaidia kutimiza malengo ya maendeleo endelevu hususani lengo la afya kwa wote ifikapo 2030.

Hivyo WHO inasisitiza mambo muhimu matano ya kuzingatia kuhusu chanjo: Mosi chanjo ni salama na inafanya kazi, pili chanjo inazuia magonjwa hatari yanayokatili maisha, tatu chanjo inaongeza kinga ya mwili dhidi ya maradhi, nne chanjo mseto ni salama na zina faida kubwa na tano endapo tutasitisha chanjo basi maradhi yatarejea.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO kila mwaka chanjo huokoa maisha ya watu kati ya milioni 2 na 3, lakini hata hivyo bado watu wengi hawafikiwi na chanjo hizo duniani huku takwimu zikionyesha mtoto 1 kati ya 7 hafaidiki na ulinzi huo muhimu wa afya.

Mhudumu wa afya anaweka alama kwa mtoto baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu nchini Sudan Kusini.
UNMISS Photo
Mhudumu wa afya anaweka alama kwa mtoto baada ya kupatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu nchini Sudan Kusini.

Endapo wigo wa utoaji chanjo utaongezeka hususan katika nchi za kipato cha chini na cha wastani WHO inasema ifikapo mwaka 2030 watu milioni 24 watakuwa wameokolewa dhidi ya kutumbukia kwenye umasikini unaochangiwa na gharama kubwa za huduma za afya.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “chanjo inaokoa maisha na kuyaboresha” na kuhakikisha lengo hilo linatimia WHO inachagiza wadau wote kuwajibika kuanzia familia, wahudumu wa afya, serikali, jumuisha ya kimataifa, asasi za kiraia na wahisani wanaoombwa kuwekeza zaidi katika mustakhbali wa jamii zao kiafya.

Mwaka 2016 watoto zaidi ya milioni 116 walichanjwa kote duniani dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo polio, surua, pepopunda, kifua kikuu na utapia mlo na milioni 62 kati yao ni kutoka katika nchi masikini kabisa duniani. Na kutokana na chanjo leo hii nchi tatu zimefanikiwa kutokomeza polio kwa zaidi ya asilimia 99 ambazo ni Afghanistan, Nigeria na Pakistan.

World Health Organisation
The Two Polio Vaccines