Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa kuna Warohingya wamehamishwa, bado maelfu hatarini: IOM

Bangladesh, mvua za Monsoon zitaathiri wakimbizi wa Rohingya.
UNHCR/Caroline Gluck
Bangladesh, mvua za Monsoon zitaathiri wakimbizi wa Rohingya.

Ingawa kuna Warohingya wamehamishwa, bado maelfu hatarini: IOM

Haki za binadamu

Zaidi ya falimia 40,000 za wakimbizi wa Rohingya walioko kwenye kambi za Cox’s Bazar nchini Bangladesh sasa zimepatiwa mafunzo ya mbinu za kuboresha makazi yao kabla ya msimu wa mvua za monsoon unaojongea kwa kasi kuanza.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM wanawake wana jukumu muhimu katika mradi huo unaoendesha na shirika hilo la uhamiaji kwa nia ya kulinda na kuokoa Maisha ya wakimbizi wakati wa zahma ya Monsoon.

Wakati mvua za kwanza zimeshaanza kuathiri makambi ya wakimbizi , IOM hivi sasa imeshakamilisha mafunzo ya kuboresha makazi, lakini inasema litaendelea kusaidia mafunzo mengine yanayotolewa na mashirika wadau.

Mafunzo hayo yanawaonyesha wakimbizi jinsi gani ya kuimarisha makambi yao ili kuhimili upepo mkali na mvua kubwa zitakazoanza kunyesha mapema mwezi Mei.

Pamoja na kutoa mafunzo hayo bado IOM inasema inahofia makambi mengine hususan yaliyofurika wakimbizi nchini Bangladesh ikisema watu hao bado wako hatarini na suluhu ya haraka inahitajika kabla ya msimu wa Monsoon kushika kasi mwezi Mei.