Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makazi mbadala kwa warohingya yakamilika- UN

Wakimbizi waRohingya nchini Bangladesh. Picha: IOM

Makazi mbadala kwa warohingya yakamilika- UN

Wahamiaji na Wakimbizi

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yanayotoa huduma kwenye kambi za wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh , leo yamekamilisha maandalizi ya eneo la kwanza jipya kwa ajili ya kuhamishia familia za wakimbizi walio katika hatari ya maporomoko yatakayosababishwa na pepo za monsuni. 

Kazi hiyo inayofanywa kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR na shirika la mpango wa chakula duniani WFP imehusisha uchimbaji wa ardhi kwa kutumia mashine kubwa na wafanyakazi zaidi ya 3500, wakiwemo wakimbizi wenyewe wa Rohingya na jamii zinazowahifadhi ili familia zilizo hatarini Cox’s Bazar ziweze kuhamia mahali salama.

Takriban familia 500 zinazoishi kwenye miinuko hivi sasa zitahamishwa. Joel Milliman ni msemaji wa IOM Geneva, Uswisi.

(Sauti ya Joel Milliman)

“Eneo hili jipya lililoandaliwa la ekari 12 liko tayari kwa ajili ya makazi na huduma nyingine muhimu kama vile na maji, huduma za kujisafi na elimu. Huku msimu wa monsuni ukikaribia tutaendelea kusaka maeneo ya ardhi na kuratibu huduma na kupata uwezo wa kufikia maeneo ili tuhakikishe tuko tayari kuchukua hatua pindi hali ya dharura itakapofika.”

Mashirika hayo yanasema kufikia hatua hii ni mafanikio makubwa yaliyotokana na ushirikiano huku msimu wa pepo za monsuni ukijongea kwa kasi.

Takriban wakimbizi 900,000 wa Rohingya wameingia Bangladesh tangu kuzuka kwa machafuko Myanmar Agosti 2017.

Na hadi sasa ombi la pamoja la mashirika ya kimataifa la kusaidia wakimbizi hao ambalo ni dola milioni 950 limefadhilia asilimia 16 tu na kuacha pengo kubwa la dola milioni 794.