Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Cameroon kuwafurusha wakimbizi wa Nigeria kunawaweka maelfu hatarini-UNHCR

Wakimbizi na wasaka hifadhi kutoka Nigeria wakiwa katika eneo la kaskazini mwa Cameroon
UNHCR/Xavier Bourgois
Wakimbizi na wasaka hifadhi kutoka Nigeria wakiwa katika eneo la kaskazini mwa Cameroon

Cameroon kuwafurusha wakimbizi wa Nigeria kunawaweka maelfu hatarini-UNHCR

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limesema linasikitishwa sana na ripoti kuhusu mamlaka za Cameroon kuwarejesha kwa nguvu maelfiu ya wakimbizi katika eneo lliloathiriwa na vurugu jimbo la Borno kaskazini mwa Nigeria. 

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema tamko lao linafuatia ripoti kwamba wakimbizi kutoka Nigeria wapatao 267 walilazimishwa kurejea nchini mwao mnamo mwezi Janurai 16 mwaka huu wa 2019. Walikuwa wamevuka kuingia Cameroon mwaka 2014.

“Tunaguswa sana na usalama na ustawi wa wanigeria wanaokimbilia Cameroon” imesema taarifa hiyo.

Inakadiriwa kuwa wanigeria 9,000 walikimbia nchi yao na kuvuka mpaka kuingia Cameroon mapema wiki hii baada ya wapiganaji kushambulia na kuiba mali katika mji mdogo wa Rann ulioko mpaka katika jimbo la Borno Nigeria. Wapiganaji walienda mbali zaidi na wakishambulia mitambo ya kijeshi, raia na vituo vya kibinadamu. Takribani watu 14 wanaripotiwa kupoteza maisha.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema "hatua hii haikutegemewa kabisa na inaweka maisha ya maelfu ya wakimbizi katika hatari. Ninaiomba Cameroon kuendeleza será yake ya milango wazi na ukarimu na kuacha mara moja kuwarejesha wakimbizi  makwao na wahakikishe wanatekeleza wajibu wao wa ulinzi wa wakimbizi chini ya sheria zake na za kimataifa"

Kwa sasa Cameroon ni nyumbani kwa wakimbizi zaidi ya 370,000, ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu 100,000 kutoka Nigeria.