Wasyria wakizidi kuumia, Urusi na Marekani waendelea kuonyeshana ubabe barazani

10 Aprili 2018

Umoja ambao Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesihi udhihirike ndani ya Baraza la Usalama ili kunusuru wananchi wa Syria unazidi kuwa ndoto kwani hata hii leo wajumbe wameendelea kuonyesha ubabe.

 

Vuta ni kuvute baina ya wajumbe wa Baraza la Usalama kuhusu sakata la madai ya matumizi ya silaha za kemikali huko Douma nchini Syria, imeendelea hii leo baada ya maazimio mawili tofauti yaliyowasilishwa mbele yao mchana wa leo Jumanne kugonga mwamba.

Azimio moja liliwasilishwa na Marekani likilenga kuanzisha jopo huru la Umoja wa Mataifa la kuchunguza matumizi ya silaha za kemikali huko Syria, ilhali azimio lingine liliwasilishwa na Urusi likilenga kuondoa ombwe la uchunguzi lililoibuka baada ya jopo la awali la uchunguzi huko Syria kutoongezewa muda.

Kila upande, yaani Urusi na Marekani, ulitumia kura yake turufu na hivyo kusababisha maazimio yote mawili  yagonge mwamba na kuwaacha wananchi wa Syria katika sintofahamu zaidi.

AZIMIO LA KWANZA

Mbele ya Baraza la Usalama hii leo mchana, Rais wa chombo hicho kwa mwezi huu wa Aprili Balozi Gustavo Meza-Cuadra kutoka Peru aliwasilisha rasimu ya kwanza ya azimio mezani, azimio lililowasilishwa na Marekani pamoja na wadau wake ikiwemo Canada, Uingereza na Ufaransa.

(Sauti ya Balozi Gustavo Meza-Cuadra)

“Matokeo ni kama ifuatavyo, 12 zimeunga mkono, 2 zimepinga na 1 hakuonyesha upande wowote. Azimio halijapita kwa sababu mjumbe mmoja wa kudumu amepinga.”

Karibu watu 400,000 wanaishi katika eneo linalozingirwa la Ghouta Mashariki, ikiwa ni asilimi 94 ya jumla ya watu wote wanaoishi maeneo yanayozingirwa nchini Syria.
UNHCR/Assadullah Amin
Karibu watu 400,000 wanaishi katika eneo linalozingirwa la Ghouta Mashariki, ikiwa ni asilimi 94 ya jumla ya watu wote wanaoishi maeneo yanayozingirwa nchini Syria.

AZIMIO LA PILI

Mjumbe aliyepinga azimio hilo ni Urusi ambayo nayo wakati ukawadia muda kwa Rais wa Baraza kuwasilisha rasimu ya azimio lililopendekezwa na Urusi.

(Sauti ya Balozi Gustavo Meza-Cuadra)

“Matokeo ya kura ni kama ifuatavyo, kura 6 zimeunga mkono, 7 zimepinga na 2 hazikuonyesha upande wowote. Rasimu ya azimio haikupita kwa kushindwa kupata idadi ya kura zinazohitajika.”

Ili azimio hilo lipite lilihitaji angalau nusu ya idadi ya kura zilizopigwa ambapo zilizounga mkono ni 6 tu ilhali 7 zimepinga.

Ingawa maazimio hayo yalishasambazwa kwa wajumbe kwa ajili ya kupitia siku za awali, kasi zaidi imeongezeka siku za hivi karibuni baada ya shambulio linalodaiwa kuwa la silaha za kemikali dhidi ya raia tarehe 7 mwezi huu huko Douma, eneo la Ghouta Mashariki nchini Syria.

AZIMIO LA TATU

Baada ya maazimio hayo mawili kugonga mwamba, kikao cha wazi cha Baraza kiliahirishwa na wajumbe wakaendelea mashauriano kuhusu rasimu nyingine ya tatu ya azimio.

Rasimu hiyo ililenga kuunga mkono jopo la kusaka ukweli kuhusu madai ya silaha za kemikali, FFM, jopo ambalo tayari limeshakwenda Syria.

Rasimu hiyo nayo ilipowasilishwa mbele ya Baraza baada ya kikao cha wazi kurejea, liligonga mwamba kwa kuwa kura hazikutosha.

Kura tano ziliunga mkno, nne zilipinga huku wajumbe sita hawakupiga kura yoyote ile.

Mwakilishi wa kudumu wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Karen Pierce alisema nchi yake haikuunga mkono azimio hilo kwa kuwa tayari jopo hilo au FFM limeshafika Syria na zaidi ya yote halina uwezo wa kubaini, kutaja au kumwajibisha mhusika.

Balozi Bashar Ja'afari, Mwakilishi wa kudumu wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama.
UN Photo/JC McIlwaine
Balozi Bashar Ja'afari, Mwakilishi wa kudumu wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa akihutubia Baraza la Usalama.

SYRIA YANYOOSHEA VIDOLE NCHI ZA MAGHARIBI

Hata hivyo mwakilishi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Bashar Ja’afari amesema wao pamoja na wao kuunga mkono uwepo wa jopo hilo nchini mwao, watahakikisha mji wa Douma umekombolewa kutoka kwa waasi ili wajumbe wa jopo hilo waweze kufika popote pale wanapotaka kufika.

Ametupia lawama nchi za magharibi akisema zinasongesha hoja ya matumizi ya silaha za kemikali huko Douma ili kufanikisha ajenda yao ya kisiasa na kuhalalisha kile alichosema ni ajenda yao ya kuingilia mamlaka ya Syria.
 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter