Wakaguzi wetu bado kuingia Douma-OPCW

Takribani wiki mbili tangu kufanyika kwa shambulio linalodaiwa kuwa la kemikali huko Douma, nchini Syria, bado wakaguzi waliopelekwa eneo hilo hawajaweze kuingia.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kupinga matumizi ya silaha za kemikali, OPCW, Ahmet Üzümcü amesema hayo leo wakati akihutubia kikao cha 59 cha baraza tendaji la OPCW huko The Hague, Uholanzi akiongeza kuwa wala hafahamu ni lini wataweza kuingia ili wakague iwapo silaha za kemikali zilitumika au la.
Amesema tarehe 16 mwezi huu uthibitisho kutoka mamlaka za usalama za Syria kuwa jeshi la Syria lilishindwa kuingia Douma na kwamba maeneo ambayo kikundi hicho cha uchunguzi, FFM kilipaswa kwenda yalikuwa chini ya udhibiti wa polisi wa kijeshi wa Urusi.
Pande hizo zilikubaliana kuwa jopo kutoka Idara ya usalama ya Umoja wa Mataifa isindikize kikundi hicho hadi eneo ambako Urusi inadhibiti ili wakaguzi wapatiwe ulinzi na polisi wa kijeshi wa Urusi.
Hata hivyo watendaji kutoka Umoja wa Mataifa walitaka wafanye ukaguzi kwanza kabla wakaguzi hao hawajaingia wakisindikizwa na Urusi, kitendo ambacho hakikuweza kukamilika baada ya watangulizi hao kuzingirwa na umati wa watu kwenye eneo na ndipo wakashauriwa waondoke.
Mkurugenzi huyo mkuu akasema katika eneo la pili, wakaguzi walikumbwa na tukio la kufyatuliwa risasi ikiwemo na kulipuliwa kwa kilipuzi na hivyo walilazimika kurejea mji mkuu wa Syria, Damascus.
Mamlaka za kitaifa Syria zitaendelea kushirikiana an mamlaka za Douma na polisi wa kijeshi wa Urusi ili kutathmini hali ya usalama.
Bwana Üzümcü amehitimisha kwa kusema kwua hawajui ni lini wakaguzi hao wataingia Douma kulingana na hali ya usalama ilivyo na kwamba ni Dhahiri shahiri kuwa wakaguzi hao wanafanya kazi katika mazingira magumu.