Afya kwa wote bado kizungumkuti

7 Aprili 2018

Katika siku ya afya duniani hii leo, Umoja wa Mataifa unaendelea kupigia chepuo haki ya msingi ya kila mtu kupata huduma ya afya popote pale alipo. Umaskini unaongezewa kasi kwani watu wanatumia fedha nyingi kwenye matibabu.

Unganeni nami kutoa wito wa kila mtu apate huduma ya afya! Ndivyo anavyohitimisha Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe wake wa siku ya afya duniani hii leo.

Bwana Guterres anasema WHO ambalo ni shirika la afya ulimwenguni lilianzishwa miaka 70 iliyopita kwa msingi kwamba kupata huduma bora ya afya ni haki ya kila mtu.

Ingawa hivyo anasema hadi leo hii bado watu wanakosa huduma muhimu za afya licha ya kauli mbiu ya afya kwa wote, UHC.

Hapa ni Yemen, wagonjwa 20 wanatumia chumba kimoja hali ambayo inahatarisha kuambukizwa magonjwa kama vile surua na mengineyo yaambukizwayo kwa njia ya hewa. Kila mtu anastahili huduma bora ya afya.
OCHA/Eman
Hapa ni Yemen, wagonjwa 20 wanatumia chumba kimoja hali ambayo inahatarisha kuambukizwa magonjwa kama vile surua na mengineyo yaambukizwayo kwa njia ya hewa. Kila mtu anastahili huduma bora ya afya.

Anasema ni wazi kuwa magonjwa hatari kama vile ndui yametokomezwa na sasa dunia iko kwenye mwelekeo wa kutokomeza polio, ni vyema kuhakikisha kuwa huduma za msingi za afya zinapatikana kwa kila mtu.

Kwa mantiki hiyo Bwana Guterres anasihi kila mtu aungane na WHO katika kuazimia upya kuhakikisha kila mtu popote pale alipo anapata huduma ya afya anayohitaji.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter