Viongozi ahadi ni deni tutimize kwa huduma ya afya kwa wote:Guterres

12 Disemba 2019

Katika Siku ya huduma za afya kwa wote, hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa  ametoa wito kwa viongozi wa dunia kutimiza ahadi waliyoitoa mwezi Septemba mwaka huu na kuhakikisha afya kwa wote ni hali halisi kwa kila mtu, kila mahali. 

Antonio Guterres katikaujumbe wake maalum wa siku hii ya kimataifa ya afya kwa wote  amesema wakati watu wengi wanapata huduma muhimu za afya kuliko hapo awali, bado wengi sana wanazikosa.

Ameongeza kuwa haikubaliki na sio haki kwamba nusu ya idadi ya watu ulimwenguni bado wanakosa kupata huduma hizi muhimu na watu milioni 100 hutumbukia katika umaskini uliokithiri kila mwaka kutokana na gharama za huduma za afya.

Amesema huduma za afya kwa mtu hazipaswi kutegemea utajiri wake au iwapo wanaweza kuishi.

Ameitaka dunia  kutanguliza mahitaji ya wale walio hatarini zaidi na walioachwa nyuma, kupitia kuongeza uwekezaji wa umma katika mnepo wa mifumo ya huduma za msingi za afya, ikiwemo mahitaji ya afya ya akili.

Pia ameitaka dunia kutambua  mzigo unaoongezeka unaosababishwa na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwenye mifumo ya afya na huduma za afya.

Amesisitiza kuwa huduma za afya kwa wote ni muhimu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, muongozo wa mustakabali bora kwa watu na sayari hivyo ametaka itimizwe ahadi ya uwekezaji katika ubinadamu, ustawi na mafanikio kwa kila mtu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter