Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa na mizozo ni Zinduna na Ambari

Picha ya UN
OCHA/Franck Kuwonu
Picha ya UN

Njaa na mizozo ni Zinduna na Ambari

Amani na Usalama

Mizozo na njaa kali vyaendelea kuambatana kwenye maeneo kadhaa duniani na kuacha watoto, wanawake, wanaume, vijana kwa wazee hoi bin taaban. Baraza la Usalama lakumbushwa wajibu wake.

Mizozo na njaa, ni mada kuu iliyojadiliwa leo kwenye Baraza la Usalama laUmoja wa Mataifa, wajumbe wakiangazia ni kwa jinsi gani vitendo vya chuki baina ya pande kinzani kwenye migogoro vinachochea ukosefu wa uhakika wa chakula.

David Beasley ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani, WFP akihutubia kikao hicho kwa njia ya video kutoka Biel, Uswisi amesema watu milioni 489 duniani wanakumbwa na njaa iliyosababishwa na binadamu.

Bwana Beasley amesema katika kila eneo la vita alilotembelea, watu walikuwa wanaomba kuwepo na amani kama wanavyoomba wapatiwe chakula.

Aliwaeleza wajumbe kuwa hebu wabonge bongo iwapo mtu hafahamu ni wapi atapata mlo ujao wa mtoto wake, mtu huyo anaweza kuchukua hatua ambayo haiwezi kufikirika.

(Sauti ya David Beasley)

“ISIS na makundi ya kigaidi yanataka kutumia chakula kama silaha ya kusajili wanachama wao au silaha ya vita. Tunadhani Baraza la Usalama, Umoja wa Mataifa na wahisani kote ulimwenguni na nchi wanachama tutumie chakula kama silaha ya ujenzi, silaha ya amani, silaha ya kuleta watu pamoja.”

Kuwepo kwa amani kunawezesha wakulima kama huyo pichani anayelima mihogo kuweza kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kuwa na uhakika wa chakula.
FAO/Giulio Napolitano
Kuwepo kwa amani kunawezesha wakulima kama huyo pichani anayelima mihogo kuweza kuendelea na shughuli za kilimo na hivyo kuwa na uhakika wa chakula.

Naye Mark Lowcock, ambaye ni mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayotoa usaidizi wa dharura, OCHA, amesema takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa idadi ya watu wenye uwezo wa kupata chakula duniani.

Hata hivyo amesema bado kuna watu wengine ambao kwao mlo wa siku ni ndoto kutokana na vita vinavyosababishwa na binadamu.

Ametaja Yemen, Sudan Kusini na Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria kuwa ni maeneo ambako bado kuna njaa kali huko Ethiopia, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC hali ya chakula inatia wasiwasi mkubwa.

(Sauti ya Mark Lowcock)

“Hakuna suluhu ya kibinadamu kwenye mizozo na sote tunafahamu kuwa amani na suluhu ya kisiasa vitaondoa mzunguko huu wa mizozo na njaa. Jukumu la msingi la Baraza hili ni amani na usalama duniani. Kwa maneno mengine, Baraza hili linaweza kuzua njaa kali isitokee tena.”