Skip to main content

Hali ya Yemen haiko katika hatihati ya kuwa zahma , tayari ni zahma kubwa:UN

Moja ya vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
UN/Eskinder Debebe
Moja ya vikao vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Hali ya Yemen haiko katika hatihati ya kuwa zahma , tayari ni zahma kubwa:UN

Amani na Usalama

Yemen inahitaji kupigwa jeki kiuchumi, usitishaji mapigano na  mshikamano wa kimataifa  mbali ya msaada wa kibinadamu endapo jumuiya ya kimataifa inataka kuepuka baa la njaa na kuwa majaji wa kuamua mtoto yupi aewe chakula na yupi akose au yupi anastahili kuishi na yupi kufa, wamesema leo viongozi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa wakihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

 

 

 

David Beasley,mkuu wa mpango wa chakula duniani, akizuru Sanaa, Yemen amabko mgorgoro mkubwa wa njaa umekuwa ukiendelea kwa mwaka sasa.
WFP/Marco Frattini
David Beasley,mkuu wa mpango wa chakula duniani, akizuru Sanaa, Yemen amabko mgorgoro mkubwa wa njaa umekuwa ukiendelea kwa mwaka sasa.

 

Akizungumza kuhusu hali ya chakula kwenye kikao hicho mkurugenzi mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP , David Beasly ameonya kwamba kuna changamoto kubwa tatu zinazohitaji suluhu ya haraka ambazo ni “Mosi uchumi wa Yemen unasambaratika, watu wa taifa hilo wameghubikwa na vita vya miaka mingi lakini kinachobadilika kwa kasi ni ni hali ya watu na kukaribia kusambaratika kwa uchumi , pili amesema ni uhakika wa chakula uko njiapanda, tunakosa fursa ya kufika nchi nzima ili kufahamu kiwango cha njaa, lakini ambacho hatukijui ni kibaya zaidi , kati ya watu milioni 28 wa Yemen tunaamini takriban milioni 12 au zaidi karibu nusu yao wanahitaji msaada. Na tatu zinahitajika haraka hatua za kibinadamu na kiuchumi, lakini ngoja niwe wazi, njaa itaendelea kuongezeka hadi pale mazingira yatakapobadilika, na yabadilike mara moja.”

Amesisitiza kuwa “endapo hatua hazitochukuliwa hasa katika suala la uchumi , sidhani kama msaada wa kibinadamu utatosheleza kukabiliana na kusambaratika kwa uchumi huo kunakoendelea. Hali hii sio kwamba iko katika hatihati ya kuwa janga , bali tayari imeshakuwa janga ambalo linatokea wakati huu tukiendelea kuzungumza.”

Mkuu wa masuala ya kibinadamu na shirika la kuratibu misaada ya dharura la Umoja wa Mataifa , OCHA Bwana. Mark Lowcock
UN Photo/Manuel Elías
Mkuu wa masuala ya kibinadamu na shirika la kuratibu misaada ya dharura la Umoja wa Mataifa , OCHA Bwana. Mark Lowcock

 

Naye mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa OCHA Mark Lowcock amekiambia kikao hicho cha Baraza la Usalama kwamba hatua zinahitajika kuchukuliwa sasa na ndio maana ameomba msaada katika masuala matano muhimu ambayo amesema endapo yote yatatekelezwa yatawanusuru mamilioni ya Wayemen na zahma kubwa.

Ombi langu la kwanza ni utekelezaji wa usitishaji mapigano katika miundombinu na vituo ambavyo vinategemewa  na operesheni za misaada na ndege za kibiashara zinazoingiza bidhaa.

Sehemu ya pili ni kuwezesha na kulinda usambazaji wa chakula na bidhaa zingine muhimu nchi nzima, kwani Yemen inaagiza karibu chakula chake chote, mafuta na madawa. Ombi la tatu ni kusaidia kuinua uchumi wa yemen kwa kuingiza fedha za kigeni na kulipa mishahara na mafao ya uzeeni.

Nne ninaomba udfadhili uongezwe na pia msaada wa operesheni za misaada. Na tano ombi langu ni wito kwa pande zote kufanya kazi na kushirikiana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya yemen ili kukomesha vita nchini humo.”

Licha ya changamoto zote hizo bado jumuiya ya kimataifa ina matumaini na Imani na watu wa Yemen kwamba amani ya taifa hilo italetwa kwa sehemu kubwa na Wayemen wenyewe.

 

Martin Griffiths, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, akilieleza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Yemen.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Martin Griffiths, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, akilieleza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Yemen.

 

Akithibitisha hilo kwenye kikao cha leo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffith amesema anaamini wako mbioni kupata suluhu ya masuala ya matayarisho ya kupunguza madhika kwa watu wa Yemen kama muafaka wa pande husika katika mzozo kuruhusu kuhamisha wagonjwa na majeruhi na kuwasafirisha nje ya Sana’a akishukuru uongozi wa muungano na serikali ya Oman kwa kukubali kusaidia masuala ya kuwezesha kusafirisha wagonjwa. Na kuhusu mjadiliano ya kupata suluhu ya kudumu ya amani amesisitiza “huu ni wakati muhimu sana kwa Yemen Nimepokea hakikisho kutoka viongozi wa pande zote za yemen kwamba wamedhamiria kuhudhuria majadiliano. Ninaamini wanasema kweli na ninawatarajia kufanya hivyo, na hali kadhalika raia wa yemen pia ambao wanataka kwa udi na uvumba suluhu ya kisiasa ya vita ambavyo vinaweka rehani maisha ya mustakabali wao kila uchao.”

Eneo lililoathirika sana na vita vinavyoendelea nchini Yemen kwa mujbu wa viongozi hao wa Umoja wa Mataifa ni Hodeydah mji ambao sasa umegeuka mahamme baada ya watu kufungasha virako kwenda kusaka usalama wao.

Na wanasema ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu na kiuchumi kwa mamilioni ya watu wanaohitaji msaada kila uchao Zaidi ya dola milioni 350 zinahitajika, kwanza kuwaepusha na baa la njaa, pili kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto wenye utapia mlo, lakini pia kutoa huduma zingine za msingi ikiwemo chakula, mishahara ya wafanyakazi wa umma, elimu, matibabu na kadhalika.