Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP laongeza usaidizi katika pembe ya Afrika

Majanga ikiwemo mabadiliko ya tabianchi yanasababisha watu kukimbiz makwao.
© UNFPA Ethiopia/Paula Seijo
Majanga ikiwemo mabadiliko ya tabianchi yanasababisha watu kukimbiz makwao.

WFP laongeza usaidizi katika pembe ya Afrika

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetangaza kuongeza usaidizi katika Pembe ya Afrika wakati huu ambapo kiwango cha njaa kinazidi kuongezeka baada ya ukame wa mfululizo, na tishio la njaa linazidi kutanda.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, zaidi ya watu milioni tisa wameingia katika uhaba mkubwa wa chakula kote katika nchi za Ethiopia, Kenya, na Somalia, na kuwaacha watu milioni 22 wakihangaika kupata chakula cha kutosha.

Mkurugenzi Mtendaji wa WFP David Beasley siku wiki iliyopita akufanya ziara katika nchi za Pembe ya Afrika ikiwemo Somalia nchi iliyokumbwa na ukame, ambako zaidi ya watu milioni saba ambao ni takriban nusu ya wakazi wake wana uhaba wa chakula na watu 213,000 tayari wanakabiliwa na hali kama ya njaa.

Muonekano wa kambi ya wahamiaji wa ADC ambayo kwa sasa inawakaribisha wakimbizi wapya wanaowasili Baidoa, Somalia.
UN Photo/Fardosa Hussein
Muonekano wa kambi ya wahamiaji wa ADC ambayo kwa sasa inawakaribisha wakimbizi wapya wanaowasili Baidoa, Somalia.

Ziarani Somalia

Upepo mkali ukivuka katika eneo kame, ni vumbi likiwa inatanda katika mahema yaliyochoka yanayokaliwa na wakimbizi wa ndani nchini Somalia. Hii ndio taswira inayomkaribisha Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP Bwana David Beasley akiwasili nchini hapa kujionea hali ya wananchi hawa.

Zaidi ya watu milioni saba idadi hii ikiwa ni takriban nusu ya wakazi wote wa Somalia wana uhaba wa chakula na watu 213,000 tayari wanakabiliwa na hali kama njaa.

Beasley alitembelea mji wa kusini wa Baardheere na kukutana na familia kadhaa ikiwa ni pamoja na watoto wenye utapiamlo na mama zao ambao wamelazimika kuacha nyumba zao na kusafiri umbali mrefu kupitia maeneo yenye mapigano kutafuta msaada wa kibinadamu.

Katika mkutano wake na kina mama hapo Beasley aliwaambia “Mabadiliko ya tabianchi yameathiri ulimwengu mzima. Na niliposimama hapa katika Pembe ya Afrika hakuna tofauti kabisa. Sasa tunaangalia watu milioni 20 wanaoandamana kifo kutokana na njaa hapa katika Pembe ya Afrika, kwakweli hapa tu niliposimama ni nchini Somalia watu milioni 7, na hiyo ni mara mbili yaidadi ilivyokuwa miezi 6 iliyopita', kwa nini? Migogoro, vikundi vya watu wenye msimamo mkali pamoja na msimu wa kiangazi ambao tumeona katika miongo kadhaa, misimu minne mitano ya kutokuwepo na mvua imetoweka, na katika miongo minne iliyopita msimu wa kiangazi ambao hatujawahi kuona kwa muda mrefu, watu wanapoteza matumaini.” 

Hata hivyo aliwapa habari njema zakuwa WFP inaongeza ufadhili mara tatu kwa idadi ya watu waliofikiwa na msaada wa chakula cha kuokoa maisha katika eneo la Baardheere, ambalo linahifadhi makumi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na ukame na migogoro.

Mama na mwanae katika kituo cha afya cha kutibu utapiamlo nchini Somalia
© UNICEF/Sebastian Rich
Mama na mwanae katika kituo cha afya cha kutibu utapiamlo nchini Somalia

Habari njema kwa wanawake na watoto

Kuongeza huko kwa msaada kunatokana na WFP kutumia fedha walizonazo pamoja na ufadhili muhimu wa dharura waliopata kutoka Ofisi ya Usaidizi wa Kibinadamu ya watu wa Marekani – USAID.

WFP inalenga kufikia watu milioni 8.5 katika Pembe ya Afrika, kutoka watu milioni 6.3 walivyokadiria mwanzoni mwa mwaka huu na watu hao watapata msaada wa chakula na fedha taslimu kwa familia, pia watasambaza  vyakula vya kuimarisha lishe kwa wanawake na watoto wadogo ili kutibu viwango vinavyoongezeka vya utapiamlo na kuzuia watu wengi zaidi kudumbukia katika njaa. 

Katika kituo cha afya wanapotoa lishe kwa watoto wenye utapiamlo mnufaika wa WFP Kame Guyo anasema msaada huo utawafaa kwani sasa wana hali tete
"Hatuna pesa za mahitaji ya kimsingi, na wakati mwingine tunalazimika kuuza mifugo yetu dhaifu iliyoathiriwa na ukame kwa bei ndogo."

WFP ikisikia kilio hicho pia imeeleza kuongeza maradufu malengo ya mpango wake wa matibabu ya utapiamlo, ikilenga kuwapa watoto wadogo na akina mama 444,000 msaada wa lishe lakini Mkuu wa WFP anasema kinachohitajika ni jamii za kimataifa kuendelea kutoa misaada kwa WFP .....
“Iwapo Mpango wa Chakula duniani tutapata usaidizi wa pesa tunazohitaji, tunaweza kuokoa maisha na tunaweza kuleta matumaini.” 

Misaada ya fedha taslimu inayotolewa na WFP pamoja na mipango ya bima pia inasaidia familia kununua chakula ili kuweka mifugo hai au kuwalipa fidia kwa wanyama wao wanapokufa.

Mwanzoni mwa mwaka huu, WFP ilionya kuwa watu milioni 13 katika Pembe ya Afrika wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana na ukame lakini kwa sasa idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka tena hadi angalau watu milioni 22 ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.