Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuepushe dharura ndani ya dharura Cox Bazar- Blanchett

Huko Cox’s Bazar, Bangladesh, Balozi mwema wa UNHCR Cate Blanchett anakutana na Jhura, mwanamke mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikimbia Myanmar pamoja na watoto wake wawili, anahofia mumewe aliuawa.
UNHCR/Hector Perez
Huko Cox’s Bazar, Bangladesh, Balozi mwema wa UNHCR Cate Blanchett anakutana na Jhura, mwanamke mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikimbia Myanmar pamoja na watoto wake wawili, anahofia mumewe aliuawa.

Tuepushe dharura ndani ya dharura Cox Bazar- Blanchett

Haki za binadamu

Balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Cate Blanchett ametaka hatua za dharura kulinda na kusaidia wakimbizi wa Rohingya walioko Bangladesh, wakati huu ambapo pepo za monsuni zinatishia usalama wao.

Bi. Blanchett ametoa wito huo baada ya ziara yake kwenye eneo la Cox Bazar mpakani mwa Myanmar na Bangladesh kumkutanisha na wakimbizi hao akiwemo mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 28 ambaye alikimbilia Bangladesh miezi 6 iliyopita baada ya kijiji chao kuvamiwa na sasa ana hofu mumewe ameuawa.

Mkimbizi huyu aitwaye Jhura Begum anaelezea hofu  yake ya sasa..

 (Sauti ya Jhura Begum)

 “Nina hofu kuwa mvua itaingia nyumbani mwangu pindi maporomoko ya udongo yatakapotokea. Nina hofu kwa sababu nina watoto wawili wadogo na hatuwezi kutenganishwa na kundi hili na kile kitakachowapata nasi kitatukumba.”

Hofu ya mkimbizi huyu na familia yake inakumba wakimbizi wengine zaidi ya 100,000 wa kabila la Rohingya ambao wanaishi kwenye makazi yaliyojaa kupita kiasi na sasa balozi mwema huyu ambaye pia ni nguli wa filamu anasaidia kupaza sauti zao.

(Sauti ya Cate Blanchett)

 “Wakimbizi wa Rohingya wamepitia ukatili mwingi na safari za kutisha kutoka Mynmar. Sasa msimu wa pepo za monsuni unapokaribia serikali ya Bangladesh, UNHCR na wadau wake wanafanya kazi kuepusha dharura ndani ya dharura.”