Utu hauna gharama, saidieni UNRWA- Guterres

15 Machi 2018

Baada ya Marekani kupunguza msaada wake kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina, UNRWA sasa harakati zinaendelea kuhakikisha  huduma za kiutu za shirika hilo zinasonga mbele na leo harakati hizo zimebisha hodi huko Roma, Italia.

Huduma za misaada zinazotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la usaidizi kwa wakimbizi wa Palestina, UNRWA zitaendelea kuwa muhimu hadi pale suluhu ya haki na ya kudumu ya mzozo kati ya Israel na Palestina itakapopatikana.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyotoa hii leo huko Roma, Italia wakati wa mkutano wa ngazi ya mawaziri wa kuonyesha mshikamano na usaidizi na UNRWA.

Amesema ziara yake huko Gaza mwaka jana ilimstaajabisha jinsi vijana walivyo na matumaini ya kushuhudia demokrasia na haki za binadamu kwa hiyo ni vyema matamanio yao yasikatishwe kwa kukatwa misaada ya UNRWA.

Badala yake amesema kwa kuzingatia huduma za UNRWA kwa wapalestina iwe ni afya, elimu, miundombinu ni vyema kuhakisha shirika hilo halikumbwi na ukata unaotokana na Marekani kupunguza msaada wake.

Pengo la sasa ni zaidi ya dola milioni 446 hivyo Katibu Mkuu anasema,

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Bila suluhu ya pamoja, UNRWA punde itakuwa haina fedha kabisa. Lazima tuepushe hali hii. Kwa kuzingatia ukata, fuko la dharura la Umoja wa Mataifa, CERF linatoa dola milioni 30.  Kwa hiyo leo nawasihi mzibe pengo hilo la mwaka 2018 kwa kutoa ahadi endelevu ya fedha.”

Bwana Guterres ameelekeza swali kwa wale wanaohoji matumizi ya UNRWA akinukuu kampeni ya changisho la fedha la shirika hilo isemayo kuwa “Utu hauna gharama.”

 

Imeandaliwa na Assumpta Massoi

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter