Hali bado iko njia panda kati ya Israeli na kundi la Kipalestina-Mladenov

20 Novemba 2019

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumatano limekutana kujadili suala la Mashariki ya Kati ambapo mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov ameonya kwamba kikao hicho kinafanyika baada ya kushuhudiwa ongezeko la machafuko kati ya Israeli na kundi la Kipalestina la Islamic Jihad huko Gaza.

Bwana Mladenova ameonya hali inasalia kuwa njia panda licha ya kupungua kwa machafuko. Hali hiyo ilichochewa na mauaji ya kulengwa ya kamanda wa kundi hilo la Kipalestina yaliyofanywa na Israeli, ambapo kwa upande wake kundi hilo lilirusha makombora zaidi ya 500 kuelekea Israeli. Navyo vikosi vya ulinzi vya Israeli vilifanya mashambulizi ya kulenga huko Gaza na kusababisha kuuawa kwa watu 34, 20 kati yao hao wakitajwa kuwa wanachama wa kundi la Kipalestina la Jihad, wanawake watatu na watoto 8.

Bwana Mladenov ameongeza kwamba, “miongoni mwa waliouwawa ni watu 8 kutoka familia moja ambao walifariki dunia baada ya shambulizi la kombora kutoka Israeli. Vikosi vya Israeli vimeripoti kwamba nyumba yao ililengwa kwa bahati mbaya. Hii inasikitisha na tukio hilo la kikatili linahitaji kuchunguzwa kwa kina na chombo huru. Hakuna halalisho la mauaji ya raia popote pale.”

Mtaalam huyo maalum ametambua juhudi za Misri katika kuhakikisha kwamba hali ya utulivu ilisalia baada ya saa 48 za uhasama. Ameongeza kwamba, “iwapo juhudi zetu zingegonga mwamba, tungekuwa katikati ya vita kubwa zaidi na mbaya kuliko mzozo wa mwaka 2014.”

Hatahivyo, bwana Mladenov amesema hatari bado inasalia na “licha ya kwamba kwa sasa mipango ya Novemba 14 inashikilia lakini makombora ya mara kwa mara yameendelea na kusababisha Israeli kujibu mashambulizi.”  Hali ambayo inahatarisha uwezekano wa ukatili zaidi.

Hatua zilizopigwa kusitisha uhasama

Bwana Mladenov amesema juhudi za Umoja wa Mataifa na wadau  katika zaidi ya mwaka mmoja na nusu zimesaidia katika kuzuia ongezeko la uhasama lakini, “Gaza hatimaye inahitaji suluhu ya kisiasa, shughuli za kijeshi haziwezi kuendelea kukwamisha uwezekano wa amani na maendeleo. Israeli haiwezi kuendelea na sera zake za uzuiaji zinazokwamisha maendeleo, viongozi wa Palestina hawawezi kuendelea kukwepa athari hatarishi za migawanyiko ya ndani ya kisiasa.”

Amesisitiza kwamba shughuli za misaada ya kibinadamu hazipaswi kupoteza lengo letu la kisiasa la kusaidia wapalestina kuendelea bila maeneo yao kukaliwa, na waisraeli kuishi kw ausalama, bila hofu ya ugaidi na mkombora. Akiongeza kwamba, “njia pekee ya kufikia lengo ni kufanya kazi na kufikia suluhu ya mataifa mawili, kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, ambapo Gaza ni sehemu muhimu ya mustakabali wa taifa la Palestina.”

Bwana Mladenov ameelezea kusikitishwa na tamko la Marekani la Novemba 18 kuhusu makazi ya Israeli katika maeneo yaliyokaliwa kutotokiuka sheria za kimataifa akisema, “msimamo wa Umoja wa Mataifa haujabadilika kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa 2334, makazi ya Israeli ni ukiukaji chini ya sheria ya kimataifa na ni kikwazo kwa suluhu la mataifa mawili na amani ya kudumu na ya haki.”

Mtaalam maalum huyo amesema shirika la Umoja wa Mataifa la msaada wa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA linakabiliwa na changamoto za kifedha na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia shirika hilo ili kuendeleza operesheni zake.

 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter