UNRWA  yapata fedha lakini zatosha mwezi mmoja tu

16 Agosti 2018

Baada ya vuta nikuvute na kutokuwa na uhakika wa ufadhili kwa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada kwa wakimbizi wa kipalestina UNRWA, hatimaye kuna matumaini baada ya baadhi ya wahisani kujitokeza kusaidia angalau shule ziweze kufunguliwa mwezi ujao.

Akizungumza kwa njia ya simu na Idhaa ya kiarabu ya Umoja wa Mataifa kutoka mjini Yerusalem, Chris Gunness ambaye ni msemaji wa UNRWA amesema baada ya kuwezeshwa na baadhi ya wahisani wana matumaini shule kuanza ijapokuwa kiasi cha fedha kilichopatikana hakitoshelezi mahitaji ya mwaka mzima.

"Shule zitafunguliwa kama ilivyopangwa na tume ya elimu ya kitaifa, ambapo zile zilizoko Ukanda wa Gaza  na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wanafungua tarehe 29 mwezi huu, wakati huko Lebanon wao ni tarehe mosi Septemba na Syria tarehe 2 Septemba," amesema Bwana Gunnes.

Pia ameongeza kuwa licha ya shule kufunguliwa kwa wakati, wana wasiwasi kwamba watoto watashindwa kuendelea kwasababu "shule zitafunguliwa mpaka  mwishoni mwa  mwezi septemba kwasababu fedha zilizopo zitaweza kuwalipa walimu elfu 20  mpaka mwishoni mwa mwezi ujao."

Mapema leo  baada ya kikao kisicho cha kawaida cha bodi ya ushauri ya UNRWA huko Amman nchini Jordan, kamishna mkuu wa UNRWA, Bwana Pierre Krähenbühl alitanganza kuwa muhula wa masomo utaanza kama kawaida kwa kwa zaidi ya wanafunzi laki Tano wa kipalestina  kwenye zaidi ya shule 711 zilizopo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, mashariki mwa Yerusalem, Gaza, Jordan, Lebanon na Syria.

Mradi wa dharura kwa elimu ulio chini ya shirika la UN la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA husaidia pia kampeni ya mwaka ya watoto kurejea shule muhula mpya wa masomo unapoanza mwezi Septemba.
UNRWA/Rushdi El-Saraaj
Mradi wa dharura kwa elimu ulio chini ya shirika la UN la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA husaidia pia kampeni ya mwaka ya watoto kurejea shule muhula mpya wa masomo unapoanza mwezi Septemba.

"Tunapotangaza leo kufunguliwa kwa mwaka wa shule, napenda kuwa wazi kwamba UNRWA haina uwezo wa kifedha. Tangu Januari 2018, UNRWA imeweza kukusanya kiasi cha dola milioni 238 fedha za ziada. Hata hivyo, kwa sasa tuna fedha za kuendesha huduma za Shirika hadi mwisho wa Septemba,” amesema Kamishna huyo wa UNRWA akiongeza kuwa “tunahitaji zaidi ya dola milioni 217 ili kuhakikisha kwamba shule zetu zisifunguliwe tu, bali pia ziweze kuendelea  hadi mwisho wa mwaka. Hii inahitaji uendelezaji thabiti wa kampeni uhamasishaji wa uchangiaji wa pamoja ulioanza tangu Januari ".

Pamoja na kuwashukuru wahisani mbalimbali Bwana Krähenbühl ametoa pongezi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  kwa jitihada zake za kuweza kuwahimiza na kuwezesha upatikanaji wa fedha hizo za awali.

Pia ameongeza  kuwa UNRWA kwa upande wake itachukuwa hatua  zinazohitajika  ili kuhakikisha fedha zinazopatikana zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya shirika  hilo, na kwa kuzingatia mipango na pia kutambua ufanisi.

Hatimaye, alithibitisha azma ya shirika hilo kudumisha na kuendeleza heshima na utu wa  wakimbizi wa kipalestina, kupitia huduma zake na mamlaka .

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter