Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya azimio, makombora yaendelea kumiminika Ghouta Mashariki

Moja ya mitaa huko Douma, eneo la Ghouta mashariki nchini Syria ambako mapigano yamesambaratisha maeneo ya makazi.
UNICEF/Amer Al Shami
Moja ya mitaa huko Douma, eneo la Ghouta mashariki nchini Syria ambako mapigano yamesambaratisha maeneo ya makazi.

Licha ya azimio, makombora yaendelea kumiminika Ghouta Mashariki

Amani na Usalama

Mapigano makali yameendelea leo asubuhi kwenye eneo la Ghouta Mashariki nchini Syria licha ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka sitisho la mapigano kwa siku 30 ili misaada ifikie wahitaji na wagonjwa waweze kuhamishwa.

Msemaji wa OCHA huko Geneva, Uswisi Jens Laerke amesema tathmini ya mashambulizi ya siku ya jumapili pekee kwenye eneo hilo inaonyesha kuwa watu 30 wakiwemo wanawake na watoto wameuawa.

Amesema Umoja wa Mataifa unajiandaa na uko tayari kupeleka misafara ya shehena ya misaada ya kuokoa maisha punde hali itakavyoruhusu huko Ghouta Mashariki na kwamba wako tayari na wana mipango ya kuhamisha mamia ya wagonjwa kadri watakavyoweza kufanya hivyo.

Siku ya Jumamosi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha kwa kauli moja azimio linalotaka sitisho la mapigano huko Ghouta Mashariki ambako mapigano ya zaidi ya wiki moja sasa yamesabisha vifo vya mamia ya raia.