Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA inasikitishwa na hali inayoendelea kuzorota Idlib, Syria

Hospitali ya wanawake na watoto jimbo la Idlib nchini Syria, ambayo ilishambuliwa kufuatia mashambulio ya anga yaliyofanyika mapema asubuhi.
© UNICEF
Hospitali ya wanawake na watoto jimbo la Idlib nchini Syria, ambayo ilishambuliwa kufuatia mashambulio ya anga yaliyofanyika mapema asubuhi.

OCHA inasikitishwa na hali inayoendelea kuzorota Idlib, Syria

Amani na Usalama

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya kibinadamu, OCHA imeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya kibinadamu inayoendelea kuzorota jimbo la Idlib Kaskazini magharibi mwa Syria ambako zaidi ya raia milioni tatu wamezuia na vita wengi wakiwa ni wanawake na watoto

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa OCHA, Jen Laerke amesema takriban raia 300,000 wamekimbia makwao kusini mwa Idlib tangu kati kati ya mwezi Desemba kufuatia ongezeko la uhasama. Hali hii inashuhudiwa wakati huu wa msimu wa baridi, hali ambayo inaweka hatarini zaidi watu ambao walikimbia makwao na nguo walizokuwa wamevaa tu.

Bwana Laerke ameongeza kwamba wengi wa waliofurushwa makwao wanaishi katika vyandarua na makazi ya muda ambako wanakabiliwa na baridi kubwa.

Ameongeza kwamba wimbi la watu waliofurushwa inaifanya hali mbaya inayoshuhudiwa Idlib kuwa mbaya zaidi kwani zaidi ya watu laki nne walifurushwa kusini mwa Idlib na takriban raia 1,300 walifariki kutokana na mashambulizi ya anga na kwamba,

(Sauti ya Jens)

“Kila siku tunapokea taarifa kuhusu familia zilizokwama katika mzozo wakisaka hifadhi na huduma zingine katika kambi ambazo tayari zimerundikana na maeneo ya miji. Wengi sasa wamesaka hifadhi katika shule, misikiti na maeneo ya umma. Tunapokea taarifa kuhusu upungufu wa chakula, makazi huduma za afya, vifaa vya msimu wa bardi na mahitaji mengine ya msingi kote Idlib. Mashirika ya kibinadamu yanakabiliwa na wakati mgumu kukabiliana na maitaji yanayoendelea kuongezeka."

Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito wake kwa pande husika kwenye mzozo kuchukua hatua stahiki kuhakikisha ulinzi wa raia kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za kimataifa. Aidha Umoja huo unarejelea wito wa Katibu Mkuu wa Desemba wa kumaliza uhasama.