Kuna uwezekano mkubwa uchaguzi DRC hautafanyika mwaka huu- Sidikou

11 Oktoba 2017

Licha ya kwamba hakuna uwezekano wa kwamba uchaguzi wa wabunge na rais utafanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hatua zimepgwa katika kuandikisha wapiga kura.

Hiyo ni kwa mujibu wa mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko DRC Maman Sidikou wakati akihutubia Baraza la Usalama kuhusu hali nchini humo hii leo akieleza kuwa huenda maafikiano kuhusu uchaguzi kufanyika mwaka huu yakagonga mwamba.

Aidha amesema hali hiyo inayoshuhudiwa nchini humo inaleta tafrani kisiasa wakati huu ambapo kuna mapigano kati ya makundi yaliyojihami na vikosi vya serikali na kusababisha hali mbaya zaidi ya kibindamu.

(Sauti ya Sidikou)

“"Kuhusiana kufanikisha uchaguzi…ingawa kuchapishwa kwa kalenda ya uchaguzi na bajeti vinasalia mambo muhimu katika mchakato wa kisiasa, na vitakuwa muhimu katika kupunguza mvutano wa kisiasa na sintofahamu kuhusu mwelekeo wa baadaye, ni muhimu kutambua kuwa hatua zimepigwa katika mchakato wa kuandikisha wapiga kura.”

Bwana Sidikou ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO amesema hadi sasa ni asilimia 6 tu ya bajeti ya kupiga kura imepatikana huku takriban wapiga kura milioni 41 wameandikishwa ambapo asilimia 48 ni wanawake.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter