Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dkt. Kanem wa Panama ateuliwa Mkuu wa UNFPA

Dkt. Kanem wa Panama ateuliwa Mkuu wa UNFPA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amemteua Dkt. Natalia Kanem wa Panama kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la idadi ya watu la umoja huo, UNFPA.

Taarifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa uteuzi huo umefanyika baada ya mashauriano kati ya Bwana Guterres na bodi tendaji ya UNFPA.

Dkt. Kanem akiwa ni mkurugenzi mtendaji wa 5 wa shirika hilo, anachukua nafasi ya Dkt Babatunde Osotimehin ambaye alifariki dunia ghafla jijini New York, Marekani tarehe 5 mwezi Juni mwaka huu.

Kabla ya uteuzi huu, Dkt. Kanem alikuwa akikaimu nafasi hiyo huku akiwa pia Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo na ni mbobezi katika masuala kadhaa ikiwemo uongozi wa kimkakati na usimamizi kwenye masuala ya tiba, afya ya umma, amani ya kimataifa na maendeleo.

Kati ya mwaka 2014 hadi 2016, Dkt. Kanem alikuwa mwakilishi wa UNFPA nchini Tanzania.