Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yachukua hatua kulinda afya ya uzazi kwa warohingya

UNFPA yachukua hatua kulinda afya ya uzazi kwa warohingya

Kufuatia ripoti kwamba miongoni mwa maelfu ya waislamu wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar wanaokimbilia Bangladesh ni wajawazito na wanawake wanaonyonyesha, shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA limechukua hatua kukidhi mahitaji yao ya afya ya uzazi.

UNFPA imesema tayari imepeleka makumi kadhaa ya wakunga wenye mafunzo maalum ya kuhudumia watu walio kwenye mazingira magumu.

Shirika hilo limemnukuu mmoja wakunga hao ajulikanaye kwa jina la Sumaya anayehudumu kwenye kambi ya Nayapara iliyoko wilaya ya Cox Bazar akisema kuwa wajawazito hao wanakabiliwa na kiwewe, hofu kwa kuwa safari ya kutoka Myanmar hadi Bangladesh ilikumbwa na machungu mengi.

Halikadhalika amesema wanahudumia wahanga wa ukatili wa kingono na kuhakikisha wanatenga maeneo salama kwa ajili ya wanawake na watoto.

image
Vikasha vyenye vifaa vya kujisafi na vile vya kusaidia wakunga wakati wa uzazi. (Picha:UNFPA/Bangladesh)
Sambamba na huduma hizo za afya ya uzazi, UNFPA inasambaza vikasha vyenye vifaa vya kujisafi pamoja na vile vya kufanikisha uzazi salama na huduma bora kwa watoto wachanga.

Asilimia 67 ya warohingya zaidi ya 370,000 waliokimbilia Bangladesh ni wanawake na wasichana ambapo kati yao hao asilimia 13 ni wajawazito na wanawake wanaonyonyesha watoto wachanga.