Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

#Myanmar acha operesheni za kijeshi dhidi ya warohingya- Guterres

#Myanmar acha operesheni za kijeshi dhidi ya warohingya- Guterres

Serikali ya Myanmar iache mara moja operesheni za kijeshi dhidi ya waislamu wa kabila la Rohingya.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António  Guterres wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala muhimu wakati huu chombo hicho kikijiandaa kwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu wiki ijayo.

image
Mzee kutoka kabila la Rohingya akiwa tayari Bangladesh baada ya kutembea kwa saa nane bila mapumziko yoyote. (Picha:UNifeed video capture)
Amesema udhalimu wa miongo kadhaa nchini Myanmar dhidi ya warohingya  haukupatiwa suluhu hadi sasa umevuka mpaka na kusababisha maelfu kukimbilia Bangladesh hivyo amesema..

(Sauti ya Guterres)

“Natoa wito kwa mamlaka za Myanmar kusitisha operesheni za kijeshi pamoja na ghasia. Halikadhalika wazingatie utawala wa sheria na kutambua haki ya kurejea kwa wale wote waliolazimika kukimbia nchi.”

Na mara baada ya kurejea, Katibu Mkuu ametaka serikali ya Myanmar…

(Sauti ya Guterres)

“Waislamu wa jimbo la Rakhine lazima wapatiwe utaifa au angalau kwa sasa wapatiwe hadhi ya kisheria itakayowaruhusu kuwa na maisha ya kawaida ikiwemo uhuru wa kutembea, kuajiriwa, elimu na huduma za afya.”

Alipoulizwa na mwandishi wa habari ni kwa namna gani anaainisha kinachoendelea Myanmar dhidi ya warohingya wakati huu ambapo Kamishna Mkuu wa haki za binadamu tayari ameita ni mauaji ya kikabila, Katibu Mkuu amesema..

(Sauti ya Guterres)

“Nitajibu swali lako kwa swali lingine. Pindi theluthi moja ya warohingya wamelazimika kukimbia nchi. Je unaweza kuwa na neno bora zaidi la kuelezea hali hiyo?”