Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kinachoendelea Myanmar ni mauaji ya kikabila- Zeid

Kinachoendelea Myanmar ni mauaji ya kikabila- Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema kinachoendelea Myanmar hivi sasa dhidi ya waislamu wa kabila la Rohingya ni sawa na mauaji ya kikabila. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Bwana Zeid amesema hayo akifungua kikao cha 36 cha Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, ikiwa ni sehemu ya mtazamo wake wa haki za binadamu katika nchi 40 duniani.

Amesema hili ni dhahiri kwa kuwa serikali ya Myanmar inazuia wachunguzi wa haki za binadamu kuingia nchini humo ili kujionea hali halisi wakati huu ambapo warohingya zaidi ya 300,000 wamekimbia nchi  yao ndani ya wiki mbili.

(Sauti ya Zeid)

“Serikali ya Mynmar iache mara moja kudai kuwa warohingya wanachoma moto nyumba zao na kumwagia taka vijiji vyao. “

Kamishna Zeid akaangazia pia viongozi wanafiki ambao wanapigia chepuo haki za binadamu nje ya nchi zao ilhali ndani hali si shwari..

(Sauti ya Zeid)

“Je haisumbui serikali kutetea haki za binadamu kwingineko ili kujionyesha kuwa wao ni watetezi duniani ilihali nyumbani wanasigina wazi haki za watu wao wenyewe? Je wanatambua kuwa huu ni unafiki?”

Hitimisho la hotuba ya Zeid ni wito kwa serikali kuwa uzingatiaji wa haki za binadamu ndio njia pekee ya kuepusha vita, ukosefu wa furaha na watu kunyimwa maslahi hivyo amesema..

 (Sauti ya Zeid)

“Ninapoendelea kuongoza ofisi hii ninahamasishwa na watu ambao wanasimama kidete kwenye nchi nyingi kutetea wale wanaoshindwa kujitetea. Hawa hawasaki madaraka wala faida binafsi, bali wanasaka haki.”