UNCDF na ENSOL wafikisha umeme Mpale, Korogwe

9 Septemba 2017
Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya mitaji na maendeleo (UNCDF), ikishirikiana na kampuni ya Ensol Tanzania Ltd. (Ensol) leo wamezindua mfumo wa umeme wa nishati ya jua katika kijiji cha Mpale kilichopo katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Mradi huo utakaonufaisha kaya 50 kati ya 730 kijiji hapo, umezinduliwa leo na Katibu Mkuu wizara ya Nishati na madini Dk. Juliana
Pallangyo.
Mkuu wa UNCDF Tanzania, Peter Malika amesema umeme ni chanzo cha maendeleo na kwamba sekta binafsi ina nafasi ya kusaidia serikali
 katika juhudi zake za kuangaza maeneo ya vijijini.
Bw Malika amesema UNCDF  itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Ensol na taasisi nyingine za umma na binafsi kuwezesha kufikisha umeme katika maeneo yanayofikika kwa shida nchini Tanzania.
Dkt. Pallangyo kwa upande wake amepongeza UNCDF na ENSOL kwa juhudi zao za ushawishi wa matumizi ya nishati mbadala mbadala ili kuboresha ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa mtu binafsi na taifa.
Mpaka sasa Ensol imeshaunganisha umeme kwa kaya 50 ambapo lengo ni kutanua mradi ili ifikapo Juni 2018 kaya 250 ziwe zimeunganishwa.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter