Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji na kupoteza makazi vyashamiri Kasai, DRC- WFP

Mauaji na kupoteza makazi vyashamiri Kasai, DRC- WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limeelezea masikitiko yake juu ya janga linaloendelea kwenye majimbo yaliyoko eneo la Kasai nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC.

(Taarifa ya Grace)

WFP inasema maelfu ya watu wameripotiwa kuuawa na kuzikwa kwenye makaburi ya pamoja na zaidi ya milioni moja wamekimbia vijiji vyao tangu mwezi Agosti mwaka jana, makumi ya maelfu wakisaka hifadhi nchi jirani ya Angola.

Jean-Pierre Kashila ni mchimbaji mdogo wa almasi ambaye amelazimika kukimbia eneo lao.

(Sauti ya Jean-Pierre)

“Tulikimbia mauaji  na tuliomba Mungu atulinde na atuweke salama. Tuliposhambuliwa, tulikimbia na kujificha kichakani.”

image
Shaka na hofu ndio vimejaa miongoni mwa wakimbizi hawa wa ndani ambao sasa hawafahamu siyo tu mustakhbali wa maisha yao bali mlo wao wa kesho. (picha:Unifeed Video)
WFP inasema raia waliokimbia ghasia wanahitaji msaada wa dharura, wengi wao wakisaka hifadhi kwa wenyeji  huko Kasai au misituni ambako hawana chakula au huduma zozote za msingi za kutosha.

Jonathan Dumont, ni msemaji wa WFP.

(Sauti ya Jonathan)

 “Jamii ya kimataifa inapaswa kuimarisha jitihada na kusaidia hawa watu. Mambo mengi yanaendelea duniani.  Jamii ya kimataifa inaombwa misaada mingi. Lakini thamani ya uhai wa watu hawa ni sawa na walio kwenye majanga mengine. Njaa inaongezeka hapa na tusipochukua hatua sasa tutajikuta kwenye hali mbaya kama ilivyo katika maeneo mengine yanayohitaji msaada wetu.”

Ghasia ziliibuka Kasai mwaka mmoja uliopita kufuatia mvutano wa kisiasa kati ya serikali kuu na Chifu wa eneo hilo, jambo lililosababisha kuundwa kwa kikundi cha wanamgambo kinachopinga serikali kiitwacho Kamuina Nsapu.