Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanaoingia Ulaya yapungua lakini ukatili wanaopata waongezeka

Idadi ya wanaoingia Ulaya yapungua lakini ukatili wanaopata waongezeka

Idadi ya wakimbizi na wahamiaji waliowasili Ulaya katika nusu ya kwanza ya mwaka huu kupitia moja ya njia tatu zinazotumika,  imepungua ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR iliyotolewa hii leo ikiangazia njia tatu za kuvuka kuingia barani humo kupitia bahari ya Mediteranea.

Sababu kuu ni kupungua kwa asilimia 94 ya idadi ya watu wanaotumia njia ya bahari kutoka Uturuki kwenda Ugiriki.

Hata hivyo ripoti inasema kwa wale wanaosafiri kutoka Afrika ya Kaskazini bado idadi imesalia kama mwaka jana ambapo wakisa safarini au wakifika Ulaya bado wanakumbwa na ukatili mikononi mwa wasafirishaji haramu au hata polisi, wengine wakikabiliana na mbwa wa polisi.

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filipo Grandi amesema kuchukua hatua kudhibiti idadi ya wakimbizi na wahamiaji wanaoingia Ulaya bila kuimarisha amani na maendeleo na njia salama za kusafiri haikubaliki kimaadili.

Grandi ametaka jamii ya kimataifa iazimie upya kuchukua hatua kuimarisha ulinzi na usalama wa wakimbizi na wahamiaji na kuweka mpango rahisi kwa wakimbizi kupata makazi na kuungana na familia zao.