Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wengine 160 watoswa baharini leo Yemen:IOM

Wahamiaji wengine 160 watoswa baharini leo Yemen:IOM

Wahamiaji wengi takribani 180 wametoswa baharini leo kwenye pwani ya Yemen na wasafirishaji haramu wa binadamu. Amina Hassan na taarifa kamili.

(TAARIFA YA AMINA)

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM maiti 6 wamepatikana huku wahamiaji wengine 13 hawajulikani walipo na 20 wakihofiwa kufa maji.

Tukio hili limefanyika siku moja tu baada ya wahamiaji wengine zaidi ya 120 kutoka Ethiopia na Somalia kutoswa baharini wakati boti waliyokuwa wakisafiria ilipokaribia pwani ya Shabwa, Yemen kwenye bahari ya Arabia na kusababisha wahamiaji wapatao 50 kuzama.

Muda mfupi baada ya kisa hicho mfanyakazi wa IOM alikuta makaburi 29 ya wahamiaji alipokuwa akifanya doria . Manusura wamesema msafirishaji haramu wa binadamu aliwatosa baharini baada ya kuona watu wa serikali karibu na pwani na sasa msafirishaji huyo amesharejea Somalia kuendelea na biashara yake.

Tangu Januari hadi sasa IOM inakadiria kwamba wahamiaji 55,000 wameondoka Pembe ya Afrika , Somalia na Ethiopia na 30,000 kati yao ni vijana wa chini ya miaka 18 huku thelithi moja wakiwa ni wasichana.