Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji umewaangusha mama na mtoto katika unyonyeshaji:UNICEF/WHO

Uwekezaji umewaangusha mama na mtoto katika unyonyeshaji:UNICEF/WHO

Unyonyeshaji ni moja ya njia muafaka na uwekezaji wa gharama nafuu unaoweza kufanywa na taifa lolote katika afya ya kizazi kipya na mustakhbali bora wa kiuchumi na jamii amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataiofa la kuhudumia watoto UNICEF Anthony Lake.

Katika mwanzo wa wiki ya unyonyeshaji duniani ambayo kila mwaka huwa Agost Mosi hadi 7, Bwana Lake amesema kushindwa kuwekeza katika unyonyeshaji , tunawaangusha kina mama na watoto na kulipa gharama mara mbili, ambayo ni kupoteza maisha na kupoteza fursa.

Hata hivyo tathimini mpya iliyotolewa leo kwa ushirikiano wa UNICEF, shirika la afya duniani WHO na mradi mpya wa kimataifa wa unyonyeshaji inaonyesha kuwa hakuna nchi inayokidhi kikamilifu viwango vya unyonyeshaji vilivyopendekezwa.

Viwango vya unyonyeshaji vilivyofanyiwa tathimini katika nchi 194 vimebaini kwamba asilimi 40 tu ya watoto walio chini ya umri wa miezi sita wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kitu kingine na nchi 23 pekee duniani ndizo zenye kiwango cha unyonyeshaji pekee wa zaidi ya asimilia 60.

Naye Dr Tedros mkurugenzi mkuu wa WHO amesema unyonyeshaji unampa mtoto mwanzo mzuri wa maisha, huku maziwa ya mama yakiwa kama chanjo ya kwanza kwa mtoto, yakimlinda na maradhi na kumpa lishe bora anayohitaji ili kuishi.

Tathimini hiyo pia imebaini kwamba uwekezaji wa dola 4.70 kwa kila mtoto mchanga unahitajika ili kuongeza kiwango cha unyonyeshaji pekee kwa watoto walio chini ya miezi sita ili kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2025.