Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto waendelea kubeba gharama za zahma Sudan-UNICEF

Watoto waendelea kubeba gharama za zahma Sudan-UNICEF

Dola milioni 22 zinahitajika haraka na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ili kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa zaidi ya watoto 100,000 nchini Sudan. Katika miezi kadhaa iliyopita shirika hilo linasema Sudan imekabiliwa na hali kadhaa za dharura ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa kuharaka katika majimbo 12 kati ya 18 ya nchi hiyo, wimbi la wakimbizi kutoka Sudan kusini na kiwango kikubwa cha utapia mlo hususani kwenye eneo la Jebel Marra jimbo la Darfur ya Kati.

Visa zaidi ya 16,600 vya kuhara vimeripotiwa huku watu 317 wakipoteza maisha, na asilimia 20 ya waathirika ni watoto amesema Abdullah Fadil mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan. Wakimbizi zaidi ya laki moja unusu wamewasili katika majimbo ya Darfur Mashariki, Darfur Kaskazini na Kusini, White Nile na Kordofan Magharibi, kati yao watoto ni 100,000.

UNICEF inasema wimbi hilo la wakimbizi ukichanganya na wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni mbili vinazidisha mzigo kwa jamii zinazowahifadhi na waathirika wakubwa wakiwa ni watoto , hivyo msaada wa haraka unahitajika kuhakikisha wanapata huduma muhimu kama maji safi na salama, usafi, afya, elimu na lishe.