Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu watamalaki Burundi, huku hofu ikitanda-UM

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu watamalaki Burundi, huku hofu ikitanda-UM

Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ukatili mwingine uliofurutu ada nchini Burundi sasa wathibitishwa. Flora Nducha na taarifa kamili.

(TAARIFA YA FLORA)

Hayo ni kwa mujibu wa tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi wa ukiukaji wa haki za binadamu Burundi iliyowasilisha taarifa yake kwenye baraza la haki za binadamu mjini Geneva Uswis Alhamisi. Wajumbe wa tume hiyo Fatsah Ouguergouz, Reine Alapini Gansou na Francoise Hampson wamesema walikwama katika uchunguzi kutokana na kutapakaa kwa hofu dhidi ya ushahidi waliokuwa wakiukusanya. Na kuongeza “leo hii tunaweza kusema kwamba hofu yetu ya awali kuhusu ukubwa na kiwango cha ukiukaji wa haki za binadamu na ukatili mwingine Burundi tangu April 2015 imethibitishwa.”

Tume hiyo imesema inasikitishwa na kushinda kupata fursa na serikali ya Burundi kutotoa ushirikiano unaotakiwa kufanikisha uchunguzi wao, lakini imefanikiwa kuwahojia raia wengi wa Bunrundi walio ukimbizini Tanzania, Rwanda, uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Kenya.Fatsah Ouguergouz ni mwenyekiti wa tume hiyo anaongeza

(SAUTI YA FATSAH OUGUERGOUZ)

“Wamepata habari zinazodai utesaji wa matumizi ya virungu, kufungwa monyororo, kuchomwa sindano za dawa zisizojulikana, kuvutwa kucha, kuvutwa sehemu za siri kwa makoleo, kuvunjwa viungo na ikiwemo vitisho vya kuuawa.”

Tangu kuanza uchunguzi wake tume hiyo imefanikiwa kukusanya ushahidi kutoka kwa watu zaidi ya 470 wa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu tangu 2015.