Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yaomboleza kifo cha ghafla cha mkurugenzi mtendaji wake

UNFPA yaomboleza kifo cha ghafla cha mkurugenzi mtendaji wake

Kwa masikitiko makubwa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA limetangaza kifo cha mkurugenzi wake mtendaji, Dr. Babatunde Osotimehin,kilichotekea ghafla usiku wa Jumapili nyumbani kwake . Alikuwa na umri wa miaka 68.

UNFPA inasema hili ni pigo kubwa kwa shirika hilo na kwa watu wote hususani wanawake, wasichana na vijana aliojitolea maisha yake kuwahudumia, tangu alipoanza kuwa Daktari nchini Nigeria.

UNFPA inatoa salamu za rambirambi kwa familia na kuwaombea ujasiri wa kuhimili msiba huu mkubwa.

image
Mwendazake Babatunde Osotimehin! Amefariki dunia leo akiwa na umri wa miaka 68.(Picha:UNFPA)
“Dr. Osotimehin alikuwa shupavu na asiyeogopa changamoto zozote na uongozi wake imara umesaidia kuiweka afya ya wanawake na wasichana katika ajenda ya kimataifa. Alielewa kwamba vijana bilioni 1.8 duniani kwa hakika ni matumaini ya mustakhbali wa dunia.

UNFPA inasema itaendeleza maono na mtazamo wa Dr. Osotimehin kwa ajili ya wanawake na vijana na itaendelea kusimama kidete kwa ajili ya haki za binadamu na utu wa kila mtu hasa vigori wasiojiweza.

Dr Osotimehin alikuwa kinara katika malengo makubwa matatu: “kuhakikisha kuna vifo sufuri vya kina mama wakati wa kujifungua, kuhakikisha kuna pengo sufuri la mahitaji ya uzazi wa mpango na kuhakikisha kuna ukeketaji sufuri kwa wanawake na wasichana”

UNFPA inamchagiza kila mmoja kuenzi maono na mtazamo wa Babatunde kwa kutekeleza malengo hayo ya kimataifa. Osotimehin, daktari na mtaalamu wa afya ya umma alikuwa mkurugenzi mtendaji wa UNFPA tangu tarehe mosi Januari 2011. Na kabla ya wadhifa huo aliteuliwa kuwa waziri wa afya wa Nigeria, baada ya baada ya kuwa mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kitaifa ya kudhibiti ukimwi nchini Nigeria.

image
Mwendazake Babatunde Osotimehin! Amefariki dunia leo akiwa na umri wa miaka 68.(Picha:UNFPA)
Dr. Osotimehin alifuzu kuwa daktari baada ya kuhitimu chuo kikuu cha Ibadan Nigeria mwaka 1972, na kisha akaenda chuo kikuu cha Birmingham, Uingereza ambako alipata shahada ya uzamifu (PHD) katika nyanja ya udaktari 1979.