Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Twasikitishwa na Marekani kujitoa mkataba wa Paris- UM

Twasikitishwa na Marekani kujitoa mkataba wa Paris- UM

Umoja wa Mataifa umesema hatua ya Marekani kujitoa hii leo kutoka mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi ni jambo la kusikitisha katika jitihada za kimataifa za kupunguza utoaji wa gesi chafuzi na kuendeleza usalama wa ulimwenguni.

Msemaji wa Umoja huo Stephane Dujarric amesema hayo alasiri hii mbele ya wanahabari akisema hatua hiyo imetangazwa na serikali ya Marekani wakati mkataba huo tayari umeanza kutekelezwa.

Amemnukuu Katibu Mkuu António  Guterres akisema kuwa Marekani ilipaswa kuwa kiongozi katika utekelezaji wa mkataba huo..

(Sauti ya Dujarric)

“Mkataba wa Paris uliridhiwa na mataifa yote duniani mwaka 2015 kwa kutambua athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi na fursa ambazo zinapatikana kwa kukabili athari hizo. Mkataba huo umetoa njia bora na mifumo ambayo inaendana na nchi zote husika.”

Amesema Katibu Mkuu ana imani kuwa miji, majimbo na sekta ya biashara ndani ya Marekani na kwingineko duniani zitaendelea kuonyesha dira na uongozi kwa kushirikiana ili kuwa na uchumi na ajira zinazojali mazingira kwa ustawi wa karne ya 21.

Kwa mantiki hiyo amesema..

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu anatarajia kushirikiana na serikali ya Marekani na wadau wote nchini humo na kwingineko duniani ili kujenga mustakhbali ambao kwao wajukuu wetu watautegemea.”