Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio Kabul laua watu 65 na mamia wamejeruhiwa

Shambulio Kabul laua watu 65 na mamia wamejeruhiwa

Zaidi ya watu 65 wameuawa na wengine zaidi ya 300 wamejeruhiwa kufuatia shambulio kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora)

Shambulio hilo limetokea baada ya mtu mmoja kufyatua kilipuzi kwenye gari kwenye eneo lenye watu wengin la Wazir Akhbar mjini Kabul ambapo ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, UNAMA, umelaani vikali huku ukituma rambirambi kwa wafiwa na kutakia ahueni ya haraka majeruhi.

Idadi kubwa ya wahanga wa shambulio hilo ni raia na idadi inatarajiwa kuongezeka sambamba na uharibifu wa mali kwa kuzingatia kuwa eneo hilo pia kuna ofisi nyingi za kibalozi.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Tadamichi Yamamoto amesema shambulio la leo ni la kigaidi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu akitaka matumizi ya vilipuzi maeneo ya raia yakome mara moja.

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Rais wa Baraza Kuu Peter Thomson ametoa kauli.

(Sauti ya Thomson)

''Mashambulizi haya ni ukumbusho yakinifu kwetu sote, kuhusu umuhimu wa jumuiya ya kimataifa kufanya kila iwezalo katika mamlaka yake, kuzuia machafuko ya misimamo mikali na kuukabili ugaidi.''