Maskini watumia pesa kununua sigara badala ya chakula, dawa na elimu- WHO

31 Mei 2017

Matumizi ya tumbaku ni tishio kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, taifa na hata kanda mbalimbali, limesema shirika la afya ulimwenguni WHO hii leo katika maadhimisho ya siku ya kupiga marufuku matumizi ya tumbaku.

Mathalani WHO imesema katika nchi za kipato cha chini na kati, kaya hutumia asilimia 10 ya mapato yake kununua bidhaa za tumbaku kama vile sigara badala ya kutumia fedha hizo kununua chakula na kulipia huduma za matibabu na elimu.

Kama hiyo haitoshi, kwenye maeneo ya kilmo cha tumbaku, asilimia kati ya 10 hadi 14 ya watoto wenye umri wa kwenda shule hawaendi shule na badala yake wanatumikishwa kwenye mashamba ya tumbaku.

Kwa upande wa afya asilimia 16 ya magonwja yasiyo ya kuambukiza, NCDs hutokana na matumzii ya tumbaku ambapo WHO inaendelea kupigia chepuo ongezeko la kodi kwenye bidhaa hizo.

Mkurugenzi Mkuu msaidizi wa WHO akihusika na NCDs Dkt. Oleg Chestov amesema kwa kutoza kodi kubwa bidhaa za tumbaku, serikali zinapata kipato na wakati huo huo kuokoa fedha ambazo zingalitumika kwa ajili ya matibabu ya magonjwa yatokanayo na matumizi ya tumbaku.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter