Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matokeo ya majaribio ya chanjo na dawa yawekwe hadharani-WHO

Matokeo ya majaribio ya chanjo na dawa yawekwe hadharani-WHO

Shirika la afya ulimwenguni WHO limewataka wadhamini wakuu wa tafiti na mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali kuzingatia viwango vipya vitakavyohitajika katika kufadhili majaribio ya dawa na chanjo kwa watu kabla hazijatumika pamoja na utolewaji wa matokeo ya majaribio hayo. Grace Kaneiya na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA GRACE)

WHO katika taarifa yake leo imesema kwamba asilimia 50 ya majaribio hayo hayatolewi hadharani mara nyingi kwa kuwa matokeo yake huwa hasi na hivyo kusababisha mitizamo mibaya kuhusu athari na faida za chanjo, dawa, na ushauri wa kitabibu hatua inayoweza kusababisha matumizi ya chini ya kiwango au haribifu ya dawa.

Katika kuhakikisha viwango tajwa vinatekelezwa, hii leo Shirika hilo la afya ulimwenguni limesema taasisi kadhaa za ufadhili wa taifiti za kitabibu, zimetoa tamko la pamoja ambapo makubaliano ni kuendeleza na kutekeleza sera katika kipindi cha miezi 12 ya ufadhili an kutangaza matokeo ya utafiti ndani ya kipindi hicho.

Mkurugenzi Msaidizi wa WHO anayehusika na mifumo ya afya na uvumbuzi Dk Marie-Paule Kieny, amesema wafadhili wa utafiti wamekubaliana kwamba hakuna visingizio vya kwanini hakuna taarifa za majaribio ya chanjo na dawa baada ya kukamilisha majaribio husika.