Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni kuwatesa raia magharibi mwa ukingo wa mto Nile-UNMISS

Acheni kuwatesa raia magharibi mwa ukingo wa mto Nile-UNMISS

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS umetoa wito kwa pande hasimu nchini humo kusitisha mateso kwa watu wake na kutekeleza majukumu yao ya kuwalinda baada ya watu 25,000 kukimbia makwao kutokana na mapigano mapya yaliyozuka siku chache magharibi mwa ukingo wa mto Nile. Taarifa kamili na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Ripoti ya UNMISS imesema maelfu wamekimbilia mji wa Aburoc, kilometa 30 kaskazini mwa mji wa Kodok ambapo takriban watu 50,000 wamekwama, wengine wakijaribu kuvuka kuelekea Sudan, wakati mapigano yaliposhika kasi Jumatano na jeshi la serikali kuchukua utawala wa eneo la Kodok..

UNMISS imesema watoa misaada walishauriwa na vikosi vya Sudan Kusini kuondoka haraka Kodok kwenda Aburoc, na UNMISS imekataliwa kuingia eneo hilo kutathmini hali halisi ya usalama. Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa UNMISS, Daniel Dickinson anasema..

(Daniel Dickinson)

"Nina wasiwasi mkubwa sana kuhusu takriban wakimbizi wa ndani 50,000 wanoshukiwa kuwa ni Aburoc. Ninatoa wito kwa serikali na vikosi vya SPLA kujizuia, kuepukana na vifo vya raia wasio na hatia na kuwalinda raia wote wa Sudan Kusini. Pia ninawahimiza wapiganaji wote wa upinzani ambao labda wamo mafichoni mjini humo wasiambatane na raia ili kuwaepusha na kulengwa"