Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machafuko ya Kasai DRC yawafungisha virago watu na kuathiri watoto

Machafuko ya Kasai DRC yawafungisha virago watu na kuathiri watoto

Machafuko yaliyozuka hivi karibuni kwenye jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) sasa yamewalazimisha watu zaidi ya 11,000 kufungasha virago na kwenda kutafuta usalama nchini Angola huku maelfu ya watoto wakiwa hatarini. Flora Nducha na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA FLORA)

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, vijiji vya mpakani nchini Angola mwezi huu wa Aprili vimeshuhudia wakimbizi 9000 ambao wamewasili na wanaendelea kuingia kila uchao wengi wakifikia Dundo Mashariki mwa Luanda mji mkuu wa jimbo la Norte.

Nalo shirika la kuhudumia watoto UNICEF linasema watoto milioni 6, idadi ya watoto wote katika majimbo matatu ya Kasai, wamo hatarini endapo vita vipya katika eneo hilo havitasitishwa.

Shirika hilo linasema watoto 300 wamejeruhiwa, 2,000 wanatumikishwa jeshini, na 4,000 wamentanganishwa na familia zao tangu mapigano hayo kuanza August 2016, na limesema hadi sasa limeweza kuwakomboa kutoka kizuizini watoto 384 waliojiunga na wanamgambo.

Dr. Tajudeen Oyewale,  Mwakilishi wa UNICEF, DRC amesema baada ya ziara yake katika eneo hilo, watoto wa Kasai wamelazimishwa kupitia madhila ya kutisha..

(Sauti ya Oyewale)

"Watoto hawa wanatakiwa kuwa majumbani mwao salama, mashuleni na katika viwanja vya michezo, si kulazimishwa kupigana katika vita, au kujeruhiwa au kuuawa katika migogoro".