Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasaka hifadhi wakumbwa na masoko ya utumwa Afrika Kaskazini

Wasaka hifadhi wakumbwa na masoko ya utumwa Afrika Kaskazini

Wahamiaji wanaotumia njia ya Libya kuelekea Ulaya ili kusaka hifadhi wameripotiwa kunasa katika mtego wa utumwa na kujikuta wakilazimika kulipa fedha nyingi ili kuweza kujinasua. Joseph Msami na taarifa kamili.

(Taarifa ya Joseph)

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesema hayo baada ya mwishoni mwa wiki kupata simulizi kutoka kwa wahanga wa mtego huo ambapo mmoja wao aliahidiwa na wasafirishaji haramu kuwa atawezeshwa kufika Ulaya.

Akitambuliwa kwa jina bandia la SC, mwanaume huyo aliwasili Niger baada ya kulipa dola 320 na baadaye kwenda Libya ambapo baada ya siku mbili alijikuta kwenye nyumba moja kunakofanyika mnada wa watumwa, wakikumbwa na vipigo huku familia zao zikipigiwa simu ili zilipe fedha waachiliwe huru.

Joe Millman msemaji wa IOM Geneva Uswisi anasema kuwa mnada unaendeshwa na raia wa Libya kwa usaidizi wa raia wa Ghana na Nigeria kwa hiyo wanachofanya sasa IOM ni kueneza ujumbe huo wa madhila kupitia mitandao na radio ili wanaotaka kufanya safari hizo wafahamu hatari zake.