Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wagonjwa wa figo Yemen wahaha kupata tiba

Wagonjwa wa figo Yemen wahaha kupata tiba

Nchini Yemen, mapigano yakiwa yanaendelea kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa Houthi miundombinu ya kiafya inazidi kusambaratika ikiacha wagonjwa taabani wakiwemo wale wa figo.

Shirika la afya ulimwenguni WHO nchini humo linasema kutokana na mapigano, wagonjwa wa figo hivi sasa wanashindwa kupata huduma ya kusafisha damu katika vituo vingine na hivyo kulazimika kwenda jimbo la Al-Hudaydah.

Mapigano yamesababisha watu wengi kukimbilia jimbo hilo na kusababisha kituo cha afya katika jimbo la Al-Hudaydah, ambacho ni moja kati ya vituo 28 nchini Yemen kushindwa kukidhi mahitaji kwa kuwa idadi ya wagonjwa ni zaidi ya 600 wakati uwezo ni wagonjwa 400.

Mwakilishi mkazi wa WHO nchini Yemen Dkt. Nevio Zagaria amesema vituo vya kutoa huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa wa ini vimezidiwa uwezo licha ya kupata vifaa vya matibabu kutoka mji mkuu Sana’a.

WHO inasema huduma hiyo ya kusafisha damu hupaswa kufanyika mara mbili kwa wiki na mgonjwa mmoja hutumia kati ya saa tatu hadi tano kukamilisha.