Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wa Ukraine waachwa kwenye madhila makubwa msimu wa baridi: O'Brien

Raia wa Ukraine waachwa kwenye madhila makubwa msimu wa baridi: O'Brien

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekutana leo kujadili hali ya Ukraine kwenye kmakao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Akiwasilisha ripoti yake kwenye kikao hicho msaidizi wa Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa kuhusu  masuala ya kisiasa Jeffrey Feltman ameeleza kuwa ni mwaka wa nne sasa vita bado vinaendelea nchini Ukraine hasa mashariki mwa nchi hiyo ambapo zaidi ya watu 10,000 tayari wamepoteza maisha wakiwemo raia na wanajeshi na zaidi ya watu 2300 kujeruhiwa. Hivyo ameongeza

(Sauti ya Feltman)

"Ukiukaji wa sitisho za mapigano umewaacha raia kwenye madhila, na kila kukicha mapigano yanavyoendelea, mzozo unakuwa mgumu kutatuliwa. Hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huu. Japokuwa nafurahia mikataba mbali mbali ikiwemo Normandy 4 lakini hakuna suluhisho la kidiplomasia. Jumuiya ya kimataifa lazima iendelee kujaribu kuleta suluhisho ili lisiwe janga. Umoja wa Mataifa unawashukuru jopo maalum la kufuatilia hali kutoka shirika la ulinzi na ushirikiano la Ulaya, OSCE."

Wakati huo huo mratibu wa masuala ya dharura wa Umoja wa Mataifa Stephen O’Brien pia akitoa ripoti yake juu ya madhila mashariki mwa Ukraine amesema ongezeko la mvutano tangu tarehe 18 mwezi uliopita,  limesababisha vifo vya wanawake wanne na madhara makubwa kwa miundombinu ya msingi na kuathiri huduma muhimu kama vile maji na umeme .

Amesema hasara hizo pamoja na baridi vimesababisha kuzorota kwa hali ya kibinadamu.

(Sauti ya O’Brien)

"Kwa mfano, hivi karibuni mifumo ya maji na umeme huko Avdiivka  imeharibiwa kwenye vurugu mnamo tarehe 29 na 30 mwezi uliopita na kwa hivi sasa Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kibinadamu wamejiunga na serikali kuongoza timu ya tathmini mjini humo tarehe kuanzia tarehe mosi mwezi huu. Walikuwa wameahidiwa usitishaji wa mapigano kwa saa kadhaa ili kutekeleza kazi yao, lakini walikuwa wanakabiliwa na mashambulizi katika maeneo yasiyo chini ya serikali. Hii ni hatari ambayo imewalazimisha kuachana na kazi zao." 

Pia  Bwana O'Brien ameonyesha wasiwasi wake kuhusu matumizi ya silaha katika maeneo ya mijini.