Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukaji wa haki DRC waongezeka 2016 ikilinganishwa na 2015- Ripoti

Ukiukaji wa haki DRC waongezeka 2016 ikilinganishwa na 2015- Ripoti

Ofisi ya pamoja ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC imesema mwaka 2016 ilipata visa 5,190 vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.

Ripoti ya ofisi hiyo imesema kiwango hicho ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na visa 4,004 mwaka uliotangulia wa 2015.

Vitendo vilivyoshamiri zaidi vya ukiukwaji wa haki nchini DRC kwa mwaka 2016 ni pamoja na kubinywa kwa demokrasia ikihusishwa zaidi na kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa ufanyike mwaka jana.

Visa vingine vilitekelezwa na jeshi la serikali FARDC kwa ongezeko la asilimia 10 ilinganishwa na mwaka 2015 ambapo majimbo ya mashariki mwa DRC ndio yaliathirika zaidi.

Katika ripoti hiyo hata hivyo, ofisi hiyo ya haki za binadamu inakaribisha hatua ya kushtakiwa kwa askari 167 wa jeshi hilo la serikali na polisi 59 wa kitaifa kwa kuhusika na ukiukaji wa haki za binadamu, DRC, kitendo ambacho ofisi hiyo imesema kinadhihirisha azma ya serikali ya kuondokana na ukwepaji wa sheria.