Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watoa wito wa utulivu hofu ya ghasia ikitanda CAR

UM watoa wito wa utulivu hofu ya ghasia ikitanda CAR

Wakati hofu ya mivutano ikitanda katika miji ya Ouaka na Bambari, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, afisa wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini humo, ametoa wito wa utulivu na kujizuia na vitendo vyovyote vitakavyoongeza hali ya ghasia kwa raia ambao tayari wako katika tafrani.

Dr. Michel Yao amesema mji wa Bambari ambao una jumla ya watu 42,000 na 26,000 kati yao wakiwa wametawanywa na machafuko mzozo mwingine itakuwa ni sawa na msumari wa moto juu ya kidonda.

Dr Yao ametoa wito kwa makundi yote yenye silaha na wadau wengine wasio serikali kutambua athari za machafuko katika hali ambayo tayari ni tete kwa watu wa mji huo.

Mapigano baina ya muungano wa waasi wa Seleka ambao wengi ni Waislam na wanamgambo wa anti-Balaka ambao wengi ni Wakristo yaliwaingiza watu milioni 4.5 wa taifa la CAR katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013.