Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udhibiti wa taka za sumu Uingereza kuangaziwa

Udhibiti wa taka za sumu Uingereza kuangaziwa

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Baskut Tuncak kesho ataanza ziara ya wiki mbili huko Uingereza kukagua jinsi nchi hiyo inavyoshughulikia dutu na taka hatarishi.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema Bwana Tuncak atakusanya taarifa kuanzia uzalishaji hadi utupaji wa taka na dutu hizo na ni jinsi gani hatua zinachukuliwa kuepusha madhara kwa binadamu kama vile wafanyakazi viwandani pamoja na mazingira.

Halikadhalika ataangalia biashara ya dutu na taka hizo na iwapo kuna sheria na mifumo ya kusimamia udhibiti wa taka zenye sumu hasa kwa kuzingatia hatua ya sasa ya Uingereza ya kujiondoa Muungano wa Ulaya, BREXIT.

Wakati wa ziara hiyo inayofuatia mwaliko wa serikali ya Uingerza, mtaalamu huyo atakutana na wawakilishi wa serikali, mashirika ya kiraia na jamii ya kibiashara na atawasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za binadamu mwezi Septemba mwaka huu.