WHO yalaani shambulio dhidi ya hospitali Syria

16 Novemba 2016

Shirika la afya duniani, WHO limelaani vikali mashambulizi dhidi ya hospitali tano nchini Syria.

Taarifa ya WHO imesema hospitali tatu kati ya hizo tano, ziko katika vijiji vilivyopo magharibi mwa Syria, ilihali mbili zipo kwenye mji wa Idleb na shambulio lilifanyika kati ya tarehe 13 hadi 15 mwezi huu wa Novemba.

Imedaiwa kwamba katika mashambulizi hayo, watu wawili wameuawa na 19 wamejeruhiwa, sita kati yao wakiwa wahudumu katika hospitali hizo.

Halikadhalika WHO imesema moja kati ya hizo hospitali zilizo magharibi wa Aleppo ziko karibu na eneo la mapigano na hivyo kuhudumia zaidi ya watu elfu kumi kwa mwezi ikiwemo upasuaji.

WHO inasisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya yamefanyika mara kwa mara tangu vita vya Syria vianze hivyo kusababisha maelfu ya wananchi ikiwemo wanawake wajawazito na watoto kukosa huduma yao ya msingi.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter