Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wito wa utulivu CAR watolewa kufuatia machafuko mapya

Wito wa utulivu CAR watolewa kufuatia machafuko mapya

Machafuko yanayoendelea na kusababisha vifo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, yameifanya ofisi ya haki za binadamu za Umoja wa Mataifa kutoa wito wa pande zote kujizuia na ghasia zaidi.

Wito huo unafuatia matukio ya hivi karibuni Kaskazini mwa nchi ambako serikali ya mpito iko madarakani baada ya miaka ya mapigano baina ya kundi la kiislam la Seleka na wanamgambo wa Kikristo wa anti-Balaka.

Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

(SAUTI YA RAVINA)

“Tunatoa wito kwa makundi yote yenye silaha na viongozi wa kisiasa vilevile wale wenye ushawishi juu ya makundi hayo nchini humo kuhakikisha kwamba hakuna machafuko zaidi yanayoendelea. Lazima kuwe na uwajibikaji wa kisheria kwa wale waliohusika na machafuko katika miezi iliyopita. "

Mapema wiki hii kwenye mji wa Kaga Bandoro, mamia ya wanachama wa kundi la ex-Seleka walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani, pia kituo cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kililengwa na jumla ya watu 18 waliuawa pamoja na wachanama 12 wa ex-seleka.