Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Balozi Affey mjumbe maalum kuhusu wakimbizi Somalia

Balozi Affey mjumbe maalum kuhusu wakimbizi Somalia

Hii leo Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filipo Grandi amemteua Balozi Mohamed Abdi Affey kuwa mjumbe wake maalum kwa masuala ya wakimbizi huko Somalia.

Taarifa ya kamishna Grandi imesema uteuzi huo utakuwa kwa kuanzia miezi sita na umezingatia msukosuko wa wakimbizi wa Somalia ambao umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya miongo miwili na kuathiri karibu vizazi vitatu vya wasomali.

Kwa sasa inahisiwa kuwa kuna wakimbizi zaidi ya milioni moja wanaoishi uhamishoni katika kanda ya Afrika huko Djibouti, Ethiopia, Kenya, Uganda na Yemen, na ilhali baadhi ya watu milioni 1.1 ni wakimbizi wa ndani.

Kamishna Grandi amesema kutokana na mafanikio ya usalama na kisiasa hivi karibuni katika maeneo nchini Somalia na pamoja na shinikizo la nchi wenyeji kuchoka kuhifadhi wakimbizi ni wakati muafaka kuanzisha upya jitihada za kupata ufumbuzi wa kudumu kwa wakimbizi na pia kutetea utunzaji wa hifadhi kwa wale wanaohitaji kuendelea na ulinzi wa kimataifa.

Balozi Affey ana uzoefu mkubwa wa kikanda, hasa kutokana na kazi yake ya awali na shirika la kiserikali linalohusika na masuala ya maendeleo pembe ya Afrika IGAD.