Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto Aleppo wamekwama kwenye jinamizi:UNICEF

Watoto Aleppo wamekwama kwenye jinamizi:UNICEF

Takriban watoto 96, wameuawa na wengine 233 kujeruhiwa Mashariki mwa Aleppo tangu Ijumaa limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. Kwa mujibu wa naibu mkurugenzi mkuu wa UNICEF Justin Forsyth watoto waliokwama Aleppo wanaishi na jinamizi, na hakuna maneno muafaka ya kuelezea madhila wanayokabiliana nayo.

Shirika hilo linasema mfumo wa afya Mashariki mwa Aleppo unasambaratika, kukiwa kumesalia madaktari 30 pekee , hakuna vifaa au dawa za dharura kutibu majeruhi na kuna ongezeko kubwa la visa vya watu kupatwa na kiwewe.

Mmoja wa Madaktari ameliambia shirika la UNICEF kwamba watoto wengi wenye fursa ndogo ya kupona mara nyingi wanaachwa na kupoteza maisha kutokana na uwezo mdogo na tiba finyu.

Forsyth amesema hakuna kinachohalalisha ukatili huo kwa watoto na kutoheshimu uhai wa mtu.

Ameongeza kuwa ateso yanayowakabili watoto Aleppo hayajawahi kushuhudiwa.