Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid aonya kuhusu kuzorota kwa haki DRC, ataka uwajibikaji kwa walosababisha vifo

Zeid aonya kuhusu kuzorota kwa haki DRC, ataka uwajibikaji kwa walosababisha vifo

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein, Alhamisi ametoa onyo kali kuhusu kuzorota kwa hali nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Amesisitiza kwamba kama sehemu ya juhudi za kuepuka janga kubwa lazima kuwe na uwajibikaji kwa mauaji ya raia na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu uliofanyika wakati wa machafuko yaliyozuka mapema wiki iliyopita.

Zeid amesema amestushwa na mlipuko wa machafuko ya karibuni mjini Kinshasa ambapo kuna raia waliuawa, wengine kujeruhiwa, makao makuu ya vyama vya siasa kuchomwa moto na kuendelea kuwepo kwa wasiwasi, akionya kwamba huenda janga kubwa liko njiani.

Watu 50 wakiwemo polisi wanne wameripotiwa kuuawa na wengine 77 kujeruhiwa , mjini Kinshasa wakati wa machafuko hayo ya Septemba 19 na 20.