Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zichukuliwe kudhibiti mfululizo wa ghasia CAR - Zeid

Hatua zichukuliwe kudhibiti mfululizo wa ghasia CAR - Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameonya kuwa hali ya usalama na haki za binadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR inaweza kuanza kuzorota tena kufuatia mfululizo wa matukio makubwa ya mizozano kwenye mji mkuu Bangui na maeneo ya vijijini.

Katika taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya haki za binadamu, Bwana Zeid ametaja tukio la tarehe 20 mwezi huu ambapo watu waliojihami walipambana na askari wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA na kusababisha vifo vya watu sita na zaidi ya raia 15 walijeruhiwa.

Halikadhalika siku hiyo hiyo, vikosi vya MINUSCA vililazimika kuingilia kati ili kunasua maafisa wa polisi wa CAR na wa Umoja wa Mataifa kutoka jengo moja mjini bangui ambalo lilikuwa limezingirwa na umati wa watu waliokuwa na hasira.

Zeid amesema hali ilivyo sasa inatia wasiwasi ikilinganishwa na mwanzo wa mwaka huu ambapo hali ilitia matumaini na kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwezi Februari.

Kamishna Zeid amesema kuna umuhimu wa kupokonya silaha vikundi vilivyojihami ambavyo vimesalia na uthabiti mkubwa na vina uwezo wa kuchochea upya ghasia.

Ametaka pia hatua ya kurejeshwa mamlaka ya serikali na utawala wa sheria sambamba na uwajibishwaji wa watuhumiwa wa matukio hayo akisema kuwa ndiyo njia ya kuhakikisha usalama kwa raia wote.